NA MWANDISHI WETU
CHAMA Cha African Democratic Alliance(ADA-TADEA) kinatarajia kugawa ardhi kwa kila mtanzania atakayefikisha umri wa miaka 21 na itakuwa marufuku kukiuza ikiwa itapata ridhaa ya kuchaguliwa na wananchi kuongoza nchi katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29,2025.
Mbali na hilo lakini pia chama hicho kimesema ni marufuku miji na vijiji kuwa na nyumba za nyasi isipokuwa maeneo ya makumbusho pekee.
Hayo yamebainika ndani ya Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025-2030 ya chama hicho iliyozinduliwa Septemba 14,2025 Mbagala mkoani Dar es Salaam muda mfupi baada ya kuzindua kampeni za urais,ubunge na udiwani ili kuwanadai wagombea wao nchi nzima.
Ilani hiyo yenye kauli mbiu “Uhuru na Uwajibikaji, Tanzania Mpya yenye Utajiri wa Haki na Amani”imeeleza kuwa katika Mabadiliko ya Upangaji wa Matumizi ya Ardhi kitu cha muhimu kwa nchi na wananchi wake ni kupanga matumizi bora ya ardhi ili kupunguza kero za uvamizi wa maeneo na vile vile kuwavunjia wananchi nyumba zao kwa kigezo cha kupanua barabara.
Ilani hiyo imefafanuwa kuwa ni vyema ardhi yote nchini ikapangiwe matumizi mtambuka ya ardhi ili kupeuka migogoro na migongano isiyokuwa ya lazima.
“Kila Mtanzania apewe kipande cha ardhi afikishapo miaka 21 ambacho kitakuwa ni mali yake na ni marufuku kukiuza.
“Hali kadhalika,iwe ni marufuku kwa Miji na Vijiji ifikapo 2030 kuwa na nyumba za nyasi labda kwa sababu maalum kama utamaduni,maenesho,kimila au matambiko lakini sio malazi”imeongeza Ilani hiyo
Ilani hiyo imeongeza kuwa iwe ni aibu kwa Taifa kuwavunjia watu nyumba au kuharibu barabara iliyojengwa kwa fedha nyingi katika kipindi kifupi na muhimu kuwa na mipango ya maono ya muda mrefu (Futuristic) itakayofafanua na kutenganisha sehemu za Kilimo,Ufugaji(Mifugo,Samaki na Nyuki),Viwanda,Miji,Vijiji,Michezo,Miundombinu na Bustani mijini na vijijini (sehemu za kupumzikia),maeneo ya uchimbaji wa madini nayo yataanishwa kuepusha usumbufu wa kuwahamisha wananchi kila wakati”imeeleza Ilani ya chama hicho.
Aidha imebainisha kuwa Mipango Miji na Vijiji itapanga matumizi bora ya ardhi kwa weledi wa hali ya juu ya kuangalia mbele miaka 100 ijayo.
“Uwezo wa kufanya hayo na wataalam tunao,vifaa vipo ni suala la kuwajibika kwa Wizara ya Ardhi na Makazi na ADA-TADEA ifaifanya miamala ya ardhi kuwa ya wazi kwa kuikamilisha na kuishughulikia kidigitali nchi nzima.
“ADA-TADEA itarekebisha sheria ya ndoa na talaka ili wote wanaume na wanawake wapate haki sawa kulingana na makubaliano.
“Endapo kutakuwa na migogoro ya ardhi na Mahakama imetupilia mbali mashauri ,itaundwa timu maalum ya kitaifa kushughulikia migogoro hiyo’’imeeleza Ilani hiyo.
Kwa upande wake Mgombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho Georges Busungu amesema Ilani hiyo inachagiza ujenzi wa Taifa la Kijamaa analolitegemea kama ilivyokuwa azima ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Sheikh Aman Abeid Karume Kiongozi wa Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
“Lengo kuu ni kuimairisha Uchumi,Uzalendo na Utaifa kwa kuiweka Tanzania kwanza kwenye fikra zetu,hali hiyo itaifanya Tanzania kuwa mpya ,kiasi ambacho watanzania wote bila ubaguzi watashiriki maendeleo yao ya Taifa .
“Ninataka Tanzania ambayo itakuwa na utajiri,haki na amaniwa kufanya mambo yake kwa kujiamini na uzingatifu wa Uhuru na Uwajibikaji wa kila mtu”amesema Bussungu”amesema Busungu
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama hicho Salehe Msumari ameelezea ilani yao kuwa ni bora kuliko za vyama vingine na kwamba ADA-TADEA kimekuwa na kuendeela kupanuka kutokana na hamu ya wananchi kujikomboa kutoka kwenye uchumi hodhi,utumwa wa fikra za ukoloni mambo leo na nguvu ya ubeberu
“Chama hiki kiliundwa kwa lengo la kuleta mabadiliko kawa amani ya kisiasa nchini Tanzania yaliyoongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Tanzania African National Union (TANU) na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa awamu ya kwanza Hayati Oscar Salathiel Kambona(1925-1997)”amebainisha Msumari



Discussion about this post