NA MWANDISHI WETU
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinatambua kuwa makazi bora ni haki ya msingi kwa kila Mtanzania na ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi hivyo kitawezesha ujenzi wa nyumba 50,000 ifikapo 2030.
Mbali na hilo lakini pia itaanzisha na kutekeleza programu maalumu ya ujenzi wa nyumba kwa makundi maalumu ya watumishi wa sekta za kitaalamu na vyombo vya ulinzi na usalama, wakiwemo walimu, polisi, madaktari, wauguzi, watumishi wa mahakama ili kuwawezesha kumiliki nyumba kabla ya kustaafu kupitia miradi ya nyumba za gharama nafuu.
Kwa mujibu wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 yenye kauli mbiu ‘’Kazi na Utu, Tunasonga Mbele’’ iliyotolewa Mei 2025 na kuzinduliwa Agost 28,2025 Kawe mkoani Dar es Salaam imebainisha kuwa CCM itaboresha Makazi ya Wananchi na Kuendeleza Miji 38.
Ilani hiyo imeeleza kuwa hivi sasa nchini Tanzania kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Tanzania ina uhaba wa nyumba 3,800,000 na uhaba huo unaongezeka kwa nyumba 300,000 kila mwaka.
Imeongeza kuwa wakati uhaba huo ukiongezeka, idadi ya watu itaongezeka kutoka watu milioni 61 (kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022) hadi kufikia watu milioni 78 ifikapo 2030.
Kupitia Ilani yake CCM imesema ili kukabiliana na uhaba wa makazi bora unaochochewa na kuongezeka kwa idadi kubwa ya watu, katika kipindi cha miaka mitano ijayo (2025 – 2030), CCM itaielekeza Serikali kuchukua hatua mahsusi za kuboresha upatikanaji wa nyumba bora, salama na za gharama nafuu kwa wananchi wa kada zote – mijini na vijijini kwa kuchukua hatua zifuatazo,
“Kutunga na kutekeleza Sera ya Nyumba na Makazi itakayokuwa Dira ya Maendeleo ya Sekta ya Nyumba na makazi nchini,
“Kutunga na kutekeleza sheria, kanuni na mikakati itakayosaidia kupunguza gharama za ujenzi ili wananchi wa kipato cha chini waweze kujenga nyumba za kisasa kwa gharama nafuu.”
“CCM kupitia Ilani yake hiyo imebainisha kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 Serikali inajenga na/au kuwezesha ujenzi wa nyumba bora na za bei nafuu zisizopungua 50,000”imefafanuwa Ilani hiyo
Ilani hiyo imefafanuwa kuwa Serikali itahakikisha kuwa maeneo yaliyopimwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makazi na biashara yanakuwa na huduma muhimu za barabara, maji, umeme na mawasiliano;
“Kuanzisha kanzidata ya kitaifa ya nyumba kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa sekta ya nyumba na kuboresha mahusiano kati ya wamiliki na wapangaji wa nyumba.
Hata hivyo Serikali watakayoiongoza itandaa mwongozo wa kitaifa utakaoelekeza mipango na ujenzi wa nyumba vijijini na mijini kwa kuzingatia mazingira na rasilimali zilizopo.
“Kuanzisha na kutekeleza programu maalumu ya ujenzi wa nyumba kwa makundi maalumu ya watumishi wa sekta za kitaalamu na vyombo vya ulinzi na usalama, wakiwemo walimu, polisi, madaktari, wauguzi, watumishi wa mahakama ili kuwawezesha kumiliki nyumba kabla ya kustaafu kupitia miradi ya nyumba za gharama nafuu.
“Kuendelea kuyaboresha makazi holela yaliyopo katikati ya miji kwa kuanzisha programu ya kuhuisha na kujenga upya na kuwamilikisha wakazi husika”imeongeza Ilani hiyo
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM na Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan,amesema Mwaka huu Taifa letu limetengeneza Dira mpya itakayoongoza mipango ya maendeleo ya nchi yetu kwa kipindi cha miaka 25 ijayo.
“CCM inaunga mkono matarajio yote yaliyoanishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, na tunaahidi kuyatekeleza kikamilifu.
“Ilani hii imezingatia kikamilifu maudhui na vipaumbele vilivyobanishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Kwa kipindi cha miaka mitano ijayo (2025-2030), CCM itaisimamia Serikali ili kuhakikisha kwamba tunaendelea kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani; kulinda amani usalama na utulivu; na kuimarisha ustawi wa Watanzania kwa kuwawezesha kiuchumi na kufungua fursa zaidi za ajira na biashara.”amesema Rais Samia



Discussion about this post