NA GOODLUCK HONGO
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG Charles Kichere amebaini kuwepo kwa migongano zaidi ya 1900 baina ya binadamu na wanyamapori iliyosababisha mauaji na uharibifu wa mali.
CAG Kichere ameyabainisha hayo katika Ripoti Kuu ya Mwaka ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 iliyotolewa tarehe 30/3/2026 .
Amesema katika mapitio yake ya Ripoti ya Utekelezaji wa Sheria za wanyamapori ya mwaka 2024/25 katika hifadhi 10 za Taifa, yamebaini matukio 1,783 ya migongano kati ya binadamu na wanyamapori.
“Migongano hii inahusu muingiliano kati ya watu na wanyamapori ambao unatokana na sababu mbalimbali ikiwemo, lakini si tu, ushindani wa rasilimali chache unaosababisha madhara kwa binadamu na wanyamapori”amesema CAG Kichere
Amesema migongano kati ya binadamu na wanyamapori ni moja ya tishio kuu kwa uhifadhi endelevu na ustawi wa watu wanaoishi jirani na maeneo yaliyohifadhiwa (madhara hayo ni pamoja na wanyama kuvamia mashamba, kuua binadamu, na kuharibu mali kama vile mashamba na mazao katika vijiji.
“Katika Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, migongano kati ya binadamu na wanyamapori iliyosajiliwa ilikuwa jumla 400.
“Matukio haya yalisababisha vifo vya wanyamapori , uharibifu wa mazao, uharibifu wa mali, majeraha, na vifo”ameongeza CAG Kichere
CAG Kichere amefafanuwa kuwa migogoro hiyo kati ya binadamu na wanyamapori ilisababishwa na shughuli za kibinadamu ndani ya mipaka ya maeneo ya hifadhi na kutokuwapo kwa vizuizi ili kuzuia wanyamapori kuvamia maeneo yenye mwingiliano mkubwa wa wanyamapori na binadamu.
“Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ilikuwa na idadi ya visa 512 katika vijiji 61,Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ilikuwa na idadi ya visa 377 katika vijiji 43 ,Hifadhi ya Taifa ya Tarangire ilikuwa na idadi ya visa 55 katika vijiji vinne,Hifadhi ya Taifa ya Saadani ilikuwa na idadi ya visa 221 katika vijiji 18 ,Hifadhi ya Taifa ya Mikumi ilikuwa na idadi ya visa 272 katika vijiji 27,Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ilikuwa na idadi ya visa 29 katika vijiji 13 ,Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ilikuwa na idadi ya visa 73 katika vijiji 12 ,Hifadhi ya Taifa ya Katavi ilikuwa na idadi ya visa 61 katika vijiji tisa,Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara ilikuwa na idadi ya visa 59 katika vijiji 38 na Hifadhi ya Taifa ya Arusha ilikuwa na idadi ya visa124 katika vijiji 12.
“Jumla idadi ya visa ilikuwa 1,783 na vijiji 237 ,Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro ilikuwa na idadi ya visa 212 katika vijiji 35,jumla kuu ni idadi ya visa 1,995 na vijiji 272.”ameongeza CAG Kichere




Discussion about this post