NA MWANDISHI WETU,KATAVI
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi,ameagiza kuharakishwa kwa miradi ya barabara, maji na umeme mkoani Katavi, huku akiwataka wakandarasi wanaosuasua kuongeza kasi ya utekelezaji ili wananchi waanze kunufaika na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali.
Maagizo hayo ameyatoa Oktoba 13,2026 wakati alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Mpanda, akiwa njiani kuelekea Sumbawanga mkoani Rukwa kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, ambapo alipata fursa ya kuwasalimia wananchi waliojitokeza kumpokea.

Akizungumzia changamoto ya umeme, Makamu wa Rais amelitaka Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kuhakikisha hadi kufikia Desemba 01, 2026, Mpanda inapelekewa Transfoma itakayoongeza megawati 50 zaidi za umeme ili kukidhi mahitaji yanayozidi kuongezeka katika Manispaa ya Mpanda na maeneo mengine ya mkoa huo.
Makamu wa Rais amesisitiza kuhakikisha ahadi ya kukamilisha maboresho hayo inatekelezwa, sambamba na kuweka nguzo za zege.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais ameonesha kutoridhishwa na kusuasua kwa ujenzi wa barabara za lami zenye thamani ya Sh. Bilioni 29, akitaka kujua sababu za kuchelewa kwa kazi licha ya wakandarasi kuwa katika maeneo ya miradi.
Ameagiza mitambo kuingizwa kazini mara moja, huku akitaka hatua za haraka zichukuliwe katika barabara ya kuelekea Kigoma, hususani eneo la Mtonyamasi ambako ujenzi wa daraja na sehemu nyingine za barabara haujakamilika, hususani kwenye kipindi hiki ambacho kumekuwa na tahadhari kubwa ya mvua za El-nino.
Pia ameelekeza kuharakishwa kwa ujenzi wa kilomita 20 za barabara inayoelekea Bandari ya Karema, akisisitiza umuhimu wa barabara hiyo katika kufungua fursa za biashara, usafirishaji na kukuza uchumi wa Katavi.
Makamu wa Rais amesisitiza matarajio ya Serikali ni kuona kazi zinakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyowekwa.
Akitoa maelezo, Mkurugenzi wa TANESCO Lazaro Twange, kuhusu mpango wa kuongeza uwezo wa umeme hadi megawati 80,ameahidi kufikia tarehe 01 Desemba miundombinu ya kuongeza umeme Mpanda itakuwa imekamilika na kutatua changamoto kubwa ya upungufu wa umeme iliyopo sasa mkoani Katavi.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, amempongeza Makamu wa Rais kwa kuwasili mkoani humo na kumwomba kufikisha salamu za shukrani kwa Rais kutokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali uliofanyika Katavi,
Amesema zaidi ya Sh.Trilioni 1.4 zimeelekezwa katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma za wananchi na kukuza uchumi wa mkoa huo.
Makamu wa Rais amewasali mkoani Katavi akiwa njiani kuelekea Sumbawanga mkoani Rukwa kumwakilisha Rais katika kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa mwaka 2026 akiwa ameambatana na Waziri wa Maji Jumaa Aweso.

Discussion about this post