NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR
MNADHIMU Mkuu wa Baraza la Wawakilishi kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Prof. Omar Fakih Hamad,ameitaka Serikali kuiangalia kwa karibu hali ya Kisiwa cha Uzi kilichopo Mkoa wa Kusini Unguja akisisitiza umuhimu wake katika uhifadhi wa mazingira na kukuza utalii.
Prof.Hamad amehimiza umuhimu wa kuchukua hatua za pamoja ili kulinda fukwe, mikoko, miti ya asili na rasilimali nyingine zinazokifanya kisiwa hicho kuwa na thamani ya kipekee.
Prof.Hamad ameyasema hayo Oktoba 13, 2026, wakati wa ziara yake ya kusikiliza changamoto na kero zinazowakabili wananchi katika kisiwa hicho ambapo shughuli za uchimbaji mchanga na ukataji wa miti zikielezwa kushamiri.
Amesema ni muhimu kwa wananchi pia kushirikiana katika kukiendeleza kisiwa chao na kulinda rasilimali zilizopo kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.
Aidha amesema wananchi wanapaswa kutambua kuwa uharibifu wa mazingira unaofanywa na baadhi ya watu ndani ya jamii unaweza kuleta madhara makubwa kwa wakazi wote wa kisiwa hicho.
“Kwa sababu wachimbaji wa mchanga na wanaokata miti ya asili wanatoka humu humu Uzi, nawaombeni sana mshirikiane kuulinda urithi wenu ambao ni muhimu kwa Taifa,”
“Madhara ya uharibifu wa mazingira yatawakumba kwanza wananchi wa Uzi wenyewe, hivyo ni kuna umuhimu wa kuchukua hatua za pamoja kulinda fukwe, mikoko, miti ya asili na rasilimali nyingine zinazokifanya kisiwa hicho kuwa na thamani ya kipekee”amesema Prof. Hamad

Wakizungumzia hali ya uharibifu wa mazingira katika Kijiji cha Uzi Kiswani baadhi ya wananchi wameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kupiga marufuku uchimbaji wa mchanga katika maeneo ya fukwe za bahari kisiwani humo, wakieleza kuwa shughuli hiyo inatishia usalama wa makazi yao na mustakabali wa kisiwa hicho.
Mmoja wa wananchi wa kisiwa hicho Omar Suleiman amesema uchimbaji wa mchanga katika fukwe za bahari umewaingiza hofu kubwa kutokana na kuongezeka kwa hatari ya maji ya bahari kufika katika makazi yao.
“Kwa kweli hii ni dalili ya kupoteza kisiwa, kwani maji ya bahari kila uchao yanakuja majumbani kwetu kutokana na uchimbaji wa mchanga ufukweni,” amesema Suleiman.
Naye Mahadhi Abdulkheiry amesema Serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka kukomesha uchimbaji wa mchanga, akionya kuwa kutokuchukua hatua kunaweza kusababisha kisiwa cha Uzi kutoweka kutokana na athari za kimazingira.
“Kila unapopita, iwe ufukweni au kwenye makazi yetu, utaona mashimo ya kila aina ambayo yametuongezea hatari kwa watoto wetu na hata sisi wazee,” amebainisha Abdulkheiry.

Kwa upande wake Marhumi Hemed Suleiman ameongeza kuwa hali ya uchimbaji wa mchanga inatia wasiwasi kuhusu usalama wa kisiwa hicho na maisha ya wananchi, akitaka hatua za haraka zichukuliwe kabla madhara hayajawa makubwa zaidi.
Mbali na uchimbaji wa mchanga, wananchi hao wameitaka Serikali kupiga marufuku uvuvi unaotumia nyavu zinazoharibu mazingira ya baharini, wakieleza kuwa unachangia uharibifu wa matumbawe na samaki wachanga.
Mselemu Ali Fumu alisema uvuvi huo una madhara makubwa kwa viumbe wa baharini na kuathiri mazingira ambayo wananchi wanayategemea kwa shughuli zao za kiuchumi.
Kisiwa cha Uzi ni miongoni mwa visiwa vidogo vya Zanzibar ambavyo vimeendelea kuhifadhi uasili wake, vikionesha utajiri wa mazingira ya asili, mandhari ya kuvutia.


Discussion about this post