NA MWANDISHI WETU,MOROGORO
WANANCHI waliovamia Hifadhi ya Msitu wa Kuni uliopo wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro na kuanzisha shughuli za ujenzi wa nyumba wametakiwa kusitisha na kuondoka mara moja katika eneo hilo ili kulinda ikolojia yake.
Kauli hiyo imetolewa leo Desemba 15 na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wilayani humo..
“Sasa tunachowaomba kwanza msimamishe ujenzi kwenye eneo la msitu ,pili tutaangalia wale ambao wamejimilikisha maeneo makubwa ili tuyagawe kwa sababu wote ni wavamizi” amesisitiza Masanja.
Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa huruma yake aliruhusu eneo la msitu lenye jumla ya hekta 2000 limegwe ili kugawiwa kwa wananchi lakini wananchi wameendelea kulivamia eneo la msitu.
“Mwaka jana tulielekeza wananchi wapangwe kwenye hekta 2000 na hiyo ni huruma ya Mheshimiwa Rais Samia, naomba tumpongeze Mama yetu ana huruma kwa sababu ilikuwa muondolewe lakini akasema hapana hawa ni wananchi wangu wapangwe” ameongeza Masanja.
Aidha amefafanua kuwa wananchi waliomo kwenye hekta 2000 zilizomegwa wakagawiwa wako kihalali na watapimiwa ardhi na kupewa hati zao lakini waliovamia wanapaswa kuondoka katika eneo hilo.Msitu wa Kuni unaomilikiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ulisajiliwa mwaka 1953 kwa tangazo la Gazeti la Serikali.





Discussion about this post