NA MWANDISHI WETU,DODOMA
MFUKO wa Mazingira wa Duniani (GEF) umesema utaendelea kufadhili miradi ya mazingira inayozunguka jamii nchini ili kuongeza kasi ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira katika maeneo ya vijijini
Hata hivyo GEF itahakikisha jamii inajishughulisha na kilimo rafiki kwa mazingira na kutolea mfano kilimo cha mbogamboga.
Hayo yamejitokeza baada ya mfuko huo kuridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia (EBARR) unaotekelezwa katika Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma na kusimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
GEF imetoa kauli hiyo Februari 15, 2022 kupitia ujumbe wa Mfuko huo ukiongozwa na Mratibu wake Kanda ya Afrika, Dkt. Ibrahima Sow wakati wa ziara ya kutembelea Mradi huo katika Vijiji vinne vya Wilaya hiyo.
Dkt. Sow amesema GEF imedhirishwa na utekelezaji wa miradi hiyo ambayo ni ujenzi wa visima virefu vinne, malambo mawili, majosho mawili, vitalu nyumba vitatu na mashine ya kukamulia alizeti ambapo miradi hiyo imeweza kuwa chanzo mbadala cha kuongeza kipato kwa wananchi.
“GEF itaendelea kufadhili miradi ya mazingira inayozunguka jamii ili kuongeza kasi ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira katika maeneo ya vijijini sambamba kuhakikisha jamii inajishughulisha na kilimo rafiki kwa mazingira na kutolea mfano kilimo cha mbogamboga.
“Miradi hii ina faida kubwa kwa wananchi wa Mpwapwa, natoa rai kwa jamii kuweza kuitunza na kuwasaidia kwa ajili ya kuleta manufaa ya sasa na kwa kizazi kijacho” amesema Dkt. Sow
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa EBBAR Kitaifa, Dkt. Makuru Nyalobi amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kusimamia vyema miradi hiyo ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao ambayo inatarajia kuwanufaisha wananchi wa vijiji vya Nghambi, Mbugani, Kiegea na Kazania.
Amebainisha kuwa Mradi huo pia unatekelezwa katika Wilaya nyingine nne ambazo ni Kaskazini ‘A’ Unguja visiwani Zanzibar,Simanjiro mkoani Manyara, Mvomero Mkoa wa Morogoro na Kishapu mkoani Shinyanga
Aidha ameongeza kuwa miradi hiyo imetekelezwa kwa kutumia mifumo ikolojia ambapo mipango ya matumizi ya ardhi imeandaliwa.
Naye Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mbugani, Aziza Mwinyimbweni amesema Serikali ya Kijiji hicho imejipanga katika kuhakikisha kuwa mradi huo unafikia malengo yaliyowekwa na Serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii ikiwemo maji safi na salama.



Discussion about this post