MOSCOW,URUSI
RAIS wa Urusi Vlamidir Putin amesema kuishinda Urusi katika kile inachoeleza kuwa ni oparesheni ya kijeshi iliyoianzisha nchini Ukraine ni jambo lisilowezekana.
Kauli ya Rais Putin inakuja wakati ambapo Rais wa Marekani Joe Biden akifanya ziara ya kushtukiza na kukutana na Rais wa Ukraine Volodimir Zelensky na kuahidi kuipatia msaada zaidi wa kijeshi ili kuishinda Urusi baada ya kuanzisha oparesheni ya kijeshi Februari 24,2022.
Akizungumza wakati wa hotuba ya kila mwaka ya hali ya taifa mbele ya mabaraza yote mawili ya bunge na makamanda wa kijeshi Februari 21,2023 jijini Moscow,Rais Putin amesema Moscow itatekeleza kwa ustadi mipango ya kijeshi na kutimiza malengo yake nchini Ukraine na nchi za Magharibi zinawajibika kubeba dhamana kikamilifu juu ya vita hivyo.
Amesema Urusi itaendelea na vita nchini Ukraine na kuyaonya mataifa ya nchi za magharibi zinazoongozwa na Marekani kuwa yanauchochea zaidi mzozo uliopo kwa mataumini ya kuishinda Urusi.
Amesema Urus i ilifanya kila inaloweza kuepusha vita lakini Ukraine ikiungwa mkono na mataifa ya magharibi ilikuwa inapanga njama za kuivamia rasi ya Crimea, eneo ambalo Moscow ililinyakua kutoka Ukraine mwaka 2014.
Rais Putin ameongeza kuwa nchi za Magharibi bado zinaendelea kumimina fedha kuunga mkono vita na nchi hizo zilianza kuifanya Ukraine kuwa mpinzani wa Urusi muda mrefu.
Nchi za Magaharibi zikiongozwa na Marekani zimekuwa zikitoa msaada mkubwa wa kijeshi kwa Ukraine ili iweze kujilinda na mashambulizi ya Urusi lakini hali imekuwa tofauti baada ya Urusi kuendeleza mashambulizi makubwa katika nchi hiyo iliyo katikati mwa Bara la Ulaya huku ikiviweka tayari vikosi vyake vya silaha za nyuklia kwa mashambulizi ikiwa usalama wake kutokana na misaada ya nchi za magharibi itahatarisha usalama wake.



Discussion about this post