NA GOODLUCK HONGO
TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) chini ya Mkurugenzi wake Dkt.Amos Nungu imetoa kiasi cha Sh.Milioni 250 kumsaidia Mbunifu na Mtafiti wa Mita za maji zinazojiendesha zenyewe ili aweze kuanzisha kiwanda.
Tume hiyo imetoa fedha hizo kwa Mbunifu na Mtafiti Wilbroad Nyirenda ambaye amebuni mita hizo zenye mfumo kama mita za umeme unazolipia kadiri unavyotumia na kiwango cha uniti ulizopata kabla ya kujizima baada ya kumalizika.
Kutolewa kwa fedha hizo ni mchango wa Serikali katika kuthamini wanasayansi wazawa ili waweze kutoa ajira kwa watanzania wenzao na kutatua changamoto zinazoikabili jamii kupitia sayansi na teknolojia ili nchi iweze kujitosheleza na wanasayansi wake.
Akizungumza na tovuti hii ya Bajeti jijini Dar es Salaam Aprili 8,2023,Mbunifu na Mtafiti Wilbroad Nyirenda amesema anaishukuru serikali kupitia COSTECH kwa kumshika mkono kwa kumpatia fedha hizo.
Nyirenda ambaye pia ni mmiliki wa Kampuni ya Nyirenda’s Company Limited inayojishughulisha na utengenezaji wa vifaa vya kieletroniki ikiwemo mita hizo za maji ambazo hutumika kulingana na fedha zilizowekwa.
Amesema bidhaa hiyo aliibuni mwaka 2020 kwa madhumuni ya kusaidia pande mbili za watumaji,wasambazaji na wazalishaji wa maji ambapo kwa wakati huo kulikuwa na upotevu wa mapato kwa asilimia 60 katika sekta ya maji.
“Niliona kulikuwa na changamoto ya kuwa na mifumo ambayo itasaidia kujua wateja ambao wamelipa na wale wasio lipa lakini pia wateja wanaohitaji huduma ya maji na wale wanaotumia maji mengi zaidi.
“Hivyo nikaona umuhimu wa kubuni mita zitakazoondoa changamoto hiyo na kubuni mita ambayo inajiendesha yenyewe yaani ukiwa ofisini unaona kiasi cha maji alichotumia mteja na hakuna haja ya kwenda kusoma mita na kukiwa na shida utaona ukiwa huko huko ofisini.
“Mteja atalazimika kununua uniti kwa kutumia mifumo ya pesa kama wanavyonunua Luku katika mitandao ya mawasilino na uniti zikiisha basi mita itajifunga na hawezi tena kutumia maji hadi alipie hivyo inarahisisha kuthibiti na kuongeza mapato”amesema Nyirenda
Nyirenda ameongeza kuwa kwa upande wa pili wananchi walikuwa wanalalamika sana kuwa wanaibiwa ama wanadhulumiwa hasa katika sekta ya maji katika mita zilizofungwa sasa hivi kwa kubambikiwa bili kuwa sio sawa na kitu wanacholipia ambacho walitumia hivyo ambapo maji hayatoki lakini mita inasoma.
“Baada ya kuona changamoto hizo ndio nikabuni hii mita sasa ambapo atafungiwa nyumbani kwake na atapewa namba za kulipia kupitia mitandao ya simu na akishalipia tu basi mita yake itasoma na ataanza kutumia maji kama kawaida hadi uniti alizonunua zitakapoisha”amesema Nyirenda
Nyirenda amefafanua kuwa gharama za mita moja zinafikia hadi Sh.350,000,500,00 na 800,000 na 850,000 na inategemea aina ya mita kwani kuna mita za binafsi na jumuiya ambazo watu wanakwenda kuchota kwa pamoja ambapo nyingine zinatumia kadi na zingine hatumii kadi.
“Nawashukuru Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ambao walikuwa wa kwanza kunisaidia na nilibuni mita hii wakati nikiwa chuo AMSET na baada ya kubuni nilipata nafasi ya kwenda kushindana kule Dodoma kupitia COSTECH katika mashindano ya MAKISATU mwaka 2020 na niliibuka mshindi wa tatu na baada ya hapo COSTECH walinipa Sh.Milioni nane ambazo nilitumia kutengeneza vitu mbalimbali vya mita hiyo na mwaka 2021 nilienda kufanya majaribio ya mita zangu kule Zanzibar.
“Niwashukuru COSTECH kwa kunipa huo mkono kunisaidia kubadilisha kutoa ubunifu kwenda kwenye vitendo halisi lakini pia COSTECH wamenisaidia kiasi cha Sh.Milioni 250 kuanzisha kiwanda kidogo cha kuzalishia hizi mita na kwenda kuzifunga”amesema Nyirenda
Nyirenda ameongeza kuwa COSTECH hawako nyuma katika kumsaidia ambapo kwa kushirikiana na Wizara ya Maji kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wameweza kuingia mkataba wa kufanya majaribio ya mita hizo kwa Tanzania nzima isipokuwa Dar es Salaam na kila mkoa watafunga mita nne za majaribio.
“Hadi sasa tumeshafunga mikoa sita ambayo ni Pwani,Tanga,Morogoro,Arusha ,Kilimanjaro,Iringa lakini tunaendelea na kazi kufunga mikoa mingine hadi itakapomalizika yote na lengo hasa ni kuujaribu mfumo lakini pia kuboresha kulingana na matumizi ya huko”ameeleza Nyirenda
Akizungumzia changamoto,Nyirenda amebainisha kuwa tatizo ni miundombinu na mshine na malighafi za kutengenezea mita hizo ambapo wanaweza wakawa na mahitaji na kitu lakini wakakosa hali inayopelekea kutumia baadhi ya vifaa visivyo na ubora ili kukamilisha bidhaa na kushindwa kufikia lengo la kutengeneza bidhaa bora.
“Changamoto nyingine ni upatikanaji wa mashine tunazotumia kutengeneza hii mita kwani nyingi ni gharama kubwa na zingine hazipo nchini hivyo tunaendelea kukabiliana na hizi changamoto kubwa mbili za mashine na malighafi”amesema Nyirenda

Awali COSTECH imewatambua wabunifu zaidi ya 2647 kuanzia mwaka 2018 hadi 2022 na imetumia zaidi ya Sh.Bilioni 4.2 ili kuendeleza ubunifu uliofanywa na watafiti wa kitanzania katika kuhakikisha kuwa unawanufaisha watanzania kwa kubadilisha maisha yao.
Takwimu hizo zimetolewa Machi 8,2023 jijini Dar es Salaam na Mwakilishi wa Afisa Uratibu wa Utafiti Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza Sayansi,Teknolojia na Ubunifu(MTUSATE) Dickson Mjarifu wakati wa Mafunzo ya Uandishi wa Habari za Sayansi,Teknolojia na Ubunifu kati ya waandishi wa habari na watafiti yaliyoandaliwa na COSTECH
Amesema kati ya wabunifu hao 283 walipatiwa msaada wa kitaalamu kutoka katika taasisi mbalimbali za kiserikali ili kuendeleza bunifu zao kwa manufaa ya nchi na watanzan ia wote
“kuanzia mwaka 2018 hadi 2022 COSTECH tumewatambua wabunifu 2647 katika ya hao 283 wamepatiwa msaada wa kitaalamu na 178 wamepatiwa fedha ili kuendeleza bunifu zao na ”amesema Mjarifu




Discussion about this post