NA MWANDISHI WETU,DODOMA
JESHI la Polisi nchini limetoa wito kwa baadhi ya Viongozi wenye taarifa za kufanyiwa uhalifu wowote wa kijinai waziwasilishe kupitia taratibu zilizopo za kisheria na kujiepusha kuandaa taarifa za uzushi na za uongo kwa nia ya kuihadaa na kuiaminisha jamii kwa mambo ambayo hayapo
Jeshi hilo limeongeza kuwa kuandaa taarufa za uzushi na za uongo ni kiashiria tosha kuwa, lengo lao si kujenga bali ni kutaka kuvuruga amani, utulivu na usalama wa nchi yetu.
Kauli ya Jeshi la Polisi imetolewa baada ya kusambaa kwa taarifa mbalimbali katika mitandao ya kijamii kuhusu matukio yaliyojitokeza wakati wa kufanyika kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 27,2024 nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Novemba 28,2024 jijini Dodoma na Msemaji wa Jeshi la hilo nchini DCP David Misime amesema zipo taarifa kwenye Mitandao ya Kijamii na Vyombo vingine inayoonyesha kutolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Katavi, Roda Kunchela ikieleza kuwa, Mgombea wa Mtaa wa Miembeni Kilimahewa kupitia Chama hicho, Nsajigwa Mwandembwa alikamatwa na Polisi akiwa nyumbani kwake.
Aidha, ameeleza kuwa, huko katika eneo la Mwamkulu,Herman Lutambi Mzee amepigwa hadi kivunjwa mkono na Diwani wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Pia katika taarifa hiyo ameeleza kuna gari ndogo iliyotaka kumteka Christopher Kapaso aliyekuwa anagombea nafasi ya uenyekiti mtaa wa Kigamboni.
DCP Misime amebainisha kuwa Jeshi la Polisi limefuatilia kwa kina ukweli wa taarifa hizo ili ikibainika ni za kweli hatua za kisheria zichukuliwe.
‘’Baada ya ufuatiliaji huo sambamba na kuchukuwa maelezo ya watu mbalimbali, imebainika taarifa hizo ni za kutengeneza na kuongeza chumvi ili kudanganya na kupata huruma ya wananchi.
‘’Ukweli uliopo kulingana na watu walioshuhudia ni kwamba Nsagigwa Mwandembwa mgombea kiti cha Mtaa wa Miembeni Kilimahewa alikuwa akifanya fujo kwenye kituo cha kupigia kura cha Miembeni na alionywa mara kadhaa lakini hakusikia.
‘’Baada ya kufikia hatua ambayo haivumiliki tena alikamatwa akiwa kwenye hicho kituo na kupelekwa kituo cha Polisi na kuhojiwa na bàada ya mahojiano na alipoona yeye mwenye athari ya vitendo vyake alidhaminiwa ili akakamilishe taratibu zake za uchaguzi kusubiri hatua zingine za kisheria.
DCP Misime ameongeza kuwa kuhusiana na taarifa aliyotoa kuwa, Herman Lutambi Mzee amepigwa na Diwani wa CCM hadi kuvunjwa mkono, ufuatiliaji wa kina umefanyika na imebainika kuwa, kilichokuwepo ni mzozo baina yao kulikosababisha kuchaniana shati na wala hajavunjwa mkono kama Mwenyekitin alivyosema
‘’Kuhusu taarifa kuwa kulikuwa na jaribio la kumteka Christopher Kapaso, taarifa hizo zimefuatiliwa na hazina ukweli wowote.
‘’Jeshi la Polisi nchini lingependa kutoa wito kwa baadhi ya Viongozi kama wana taarifa za kweli kufanyiwa uhalifu wowote wa kijinai waziwasilishe kupitia taratibu zilizopo za kisheria na kujiepusha kuandaa taarifa za uzushi na za uongo kwa nia ya kuihadaa na kuiaminisha jamii mambo ambayo hayapo kwani ni kiashiria tosha kuwa, lengo lao si kujenga bali ni kutaka kuvuruga amani, utulivu na usalama wa nchi yetu’’amesema DCP Misime



Discussion about this post