NA GOODLUCK HONGO
TAREHE 20 ya kila mwaka,dunia huadhimisha siku ya Nyuki baada ya Umoja wa Mataifa (UN) kuipanga rasmi kutokana na umuhimu wa mdudu huyo.
Lengo kuu ya kuadhimisha siku hiyo ni kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa nyuki katika mfumo wa ikolojia,kuchavusha mimea na mchango wao mkubwa katika usalama wa chakula ambapo huchangia moja ya tatu ya uzalishaji wa chakula chote duniani.
Nyuki wanatajwa kuwa ni wadudu wanaoishi kwa kushirikiana wakiwa katika kundi moja ambapo ndani ya kundi hilo kuna Malkia ambaye ni mama wa nyuki wote ndani ya kundi hilo na kazi yake ni kutaga mayai pekee ambapo pia kuna nyuki wanaoelezwa kuwa ni wa kike na ndio wengi zaidi kuliko wote wakiwa na kazi nyingi ikiwemo kumlisha malkia,kulinda mzinga,kutengeneza masega na nyingine nyingi huku nyuki wa kiume ambao ni wachache na kazi yao ni kumpanda malkia.
Mbali na hilo lakini pia Nyuki wanaelezwa kutambuana kwa kutumia harufu inayotolewa na malkia wa kundi lao kutokana na kuishi kifamilia hivyo kila kundi lina malkia wake anayedaiwa kutoa harufu tofauti na malkia wa kundi lingine.
Nyuki pia hujulikana sana kwa kutoa asali na nta kwa jamii licha ya kuwa mdudu huyo ana mazao mengine mengi nje ya asali na nta ambayo yanafaida kubwa kwa afya na mazingira yanayomzunguka binadamu.
Pamoja na umuhimu wa Nyuki katika kutoa asali lakini pia nyuki ana kitu kingine muhimu ambacho ni sumu anayotumia kujilinda dhidi ya maadui zake.
Sumu hiyo ambayo huhifadhiwa katika mkia wake ni ngumu kuivuna kutokana na mazingira ya mdudu huyo jamii ya mende hivyo inahitajika teknolojia kuweza kuivuna tofauti na asali.
Hata hivyo Tanzania ipo katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2050 ambayo inaeleza kuwa ni dhamira thabiti ya kuhakikisha kuwa ukuaji wa Uchumi nchini wenye thamani ya dola za kimarekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050 utafikiwa kwa kutekeleza msingi mkuu wa utawala bora,amani,usalama, utulivu na mifumo madhubuti inayochochea ukuaji jumuishi na endelevu.
Katika hotuba yake ya uzinduzi wa Dira ya Maendeleo 2050 Julai 17,2025 jijini Dodoma Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan anasema wanapozindua Dira 2050 watanzania wanapaswa kujielekeze katika vitendo zaidi kuliko maneno.
“Wazee wetu walisema lisilo budi hutendwa, hawakusema lisilo budi husemwa, sasa sote, Serikali, sekta binafsi na wananchi, tutende zaidi kuliko kusema.
“Hii ina maana kwamba mtihani halisi wa Dira hii utakuwa kwenye utekelezaji wake, ni lazima tufikiri, tupange na tutende kimkakati.
“Misingi tuliyofundishwa ni kwamba “Kupanga ni kuchagua.” Kwa kuzingatia dhana hiyo, Dira 2050 imebainisha vigezo mahsusi vitano vya kuchagua sekta za vipaumbele.”anasema Rais Dkt Samia
Rais Dkt Samia anabainisha kuwa Vigezo hivi ni uwezo wa kuzalisha ajira kwa wingi; uwezo wa kuongeza mauzo ya nje; uwezo wa kuchochea ukuaji wa sekta nyingine; uwezo wa kuongeza thamani hapa nchini; na uwezo wa kukuza mapato ya Serikali.
“Kwa msingi wa vigezo hivi, Dira 2050 imechagua sekta za kimageuzi tisa kwa hatua ya sasa na sekta hizi ni Kilimo, Utalii, Viwanda, Ujenzi, Madini, Uchumi wa buluu, Michezo na Ubunifu, Huduma za kifedha, na Sekta ya huduma.
“Nataka nisisitize tena, pamoja na vigezo hivi, thamani ya kweli ya Dira 2050 itapimwa kwa uwezo wetu wa kuitafsiri kwa vitendo, katika mipango, bajeti na maamuzi mbalimbali.
“Kwa hivyo, hatuna budi kuzingatia suala la uwajibikaji wa pamoja”anasema Rais Dkt.Samia
Kutokana na mazingira hayo Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imekuwa ikitekeleza Dira hiyo kwa vitendo kwa kuendeleza tafiti na bunifu za kisayansi zinazofanywa na watanzania ili kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
COSTECH imekuwa daraja muhimu kati ya wabunifu na watafiti katika kuibua kazi zao hadi kufikisha ndoto za watanzania hao katika kutengeneza mfumo unaofanya kazi na kuziweka hadharani tafiti ba bunifu hizo ili wananchi waweze kunufaika nazo.
Hata hivyo ufadhili wa COSTECH umefanikiwa kuibua bunifu na tafiti nyingi ambapo moja kati ya hizo ni mfumo wa kuvuna sumu ya nyuki.
Mfumo huo unaoelezwa kuwa ni wa kitaalamu bila kumdhuru nyuki anapotoa sumu hiyo umefanywa na kijana wa kitanzania anayejulikana kama Patrick Kitosi.
Akizungumzia na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki kuhusu ubunifu na utafiti wake wa kutengeneza mfumo wa kuwaudhi nyuki ili watoe sumu,Mkurugenzi wa Kampuni ya Sensor Tanzania Ltd Patrick Kitosi anasema wao waligundua nafasi kubwa iliyokuwepo kwa wakulima wengi nchini ambao hujikita zaidi katika kufuga Nyuki kwa ajili ya asali lakini mdudu huyo ana vitu vingine vingi zaidi ya hicho kama ilivyozeleka.
Anasema sababu nyingine iliyowafanya wafanye utafiti na kisha kuja na mfumo huo ni kuona baadhi ya nchi nyingi zenye teknolojia ya kutengeneza madawa hawana maeneo ya makubwa ya kilimo na wala hawafanyi ufugaji.
Anasema nchi hizo zinategemea kuchukua malighafi kutoka katika nchi ambazo zina mashamba na maeneo mengi ambako ufugaji wa nyuki unafanyika kama Tanzania.
“Nyuki anatoa Asali,Nyuki anatoa maziwa,Nyuki anatoa sumu ya nyuki,Nyuki anasaidia uchavushaji katika mazao,Nyuki anatoa gundi na Nyuki pia anatoa Nta”anasema Kitosi
Anasema kati ya vitu vyote hivyo ambavyo Nyuki anatoa,kitu chepesi kukivuna ni asali pekee ambapo mkulima yeye anaweka Mzinga wake na baadaye anasubiri kuja kutoa masega na kuchukua asali.
“Kati ya vitu vyote hivyo ni kimoja tu ndio utakivuna kwa urahisi na ndio maana wakulima wengi wanakimbilia asali lakini hivi vingine vyote vilivyobakia vinahitaji teknolojia kuvivuna.
“Sisi tulijikita katika teknolojia kwa sababu tuligundua sio kwamba wakulima hawapendi kuvuna vitu hivyo vingine vyote lakini wanakosa teknolojia au watu wa kuwaletea teknolojia ,au kuwapa elimu juu ya hizo teknolojia za kuvuna hivyo vitu vingine.
“Na ndio maana sisi tuliona umuhimu wa kuwekeza kwenye huo mfumo,hivyo kuvuna maziwa ya Nyuki inahitajika teknolojia kuyavuna lakini nani sasa anayeingiza hizo teknolojia au mfumo wa kuvuna vitu hivyo?”anasema Kitosi

Kitosi ambaye kielimu ni Mhandisi anabainisha kuwa mataifa mengine duniani yanafaidika na mazao hayo ya nyuki hivyo na wao wanajaribu kuona wakulima wa kitanzania nao wanafaidika na mazao yote anayotoa nyuki kama yalivyo mataifa mengine kwa kuwapatia mifumo au teknolojia nzuri,bora na nyepesi kuitumia na kwa gharama ndogo.
Anaeleza kuwa ili uvune sumu ya nyuki ni lazima uwakasirishe na wakishakasiria ndipo watakuja kuuma na kutoa hiyo sumu.
“Sisi tulianza kufanya utafiti tangu 2021 ndipo tulipokuja na njia ya kuwaita Nyuki waje wakusanyike mahali na baadaye hiyo sehemu wanayokusanyika ndio kuna kuwa mfumo wa kuwashtua ili kuwaudhi.
Anaongeza kuwa mashine zao zinatumia teknolojia ya electronic na umeme ambapo zinatoa mawimbi madogo(Frequency) ambayo Nyuki wanayasikia na wanavutiwa na hayo mawimbi na kisha wanasogea katika hicho kifaa cha umeme au mashine.
“Bahati mbaya sasa sehemu ambayo wanasogea na kuigusa wanakuwa wanashtushwa na shoti ya umeme,sasa ile shoti ya umeme ikiwashtua wanakasirika,na wakikasirika wanakuwa wanatafuta namna ya kujilinda na hapo ndio sasa wanang’ata hicho kifaa na wakati wanang’ata ndipo sasa wanaachia ile sumu inayopatikana katika mikia yao”anafafanuwa Kitosi
Kitosi anaeleza kuwa shoti inayotumika kuwashtua haina madhara kwao na ndio maana wanarudi na kuuma na kisha wataiacha kwa muda ili sumu ikusanyike na baadaye kuikusanya sumu hiyo na na kuipima kwa gram kwa ajili ya kwenda kuuzwa.
“Baadhi ya watu hasa kwenye nchi zingine wao wanafanya kazi hii ya kuvuna tu sumu inayopatikana kwenye nyuki na kuwauzia watu wanaotengeneza dawa.
“Sasa sisi tumegundua changamoto hapa nchini kwamba tunao wakulima wengine na wafugaji wa nyuki lakini bado hii fursa ya kuvuna hiyo sumu na kuiuza huko nje bado hawajaingia na kuichangamkia na changamoto kubwa ni elimu ya watu kutojua kitu kama hicho lakini pia hata wanaofahamu hawapati vifaa vinavyowasaidia kufanya hiyo kazi na ndio maana sisi tukaona kwamba tuanze na kutatua changamoto ya kwanza ya upatikanaji wa hivyo vifaa na kufanya utafiti namna ya kupata hiyo sumu kwa kutumia teknolojia na mazingira tuliyonayo hapa nchini.
“Ndipo tulipokuja na huu ubunifu wa kutengeneza hizi mashine kwa ajili ya kuvunia hiyo sumu inayopatikana kutoka kwenye nyuki na uvunaji wake huchukua nusu saa tu na kisha unaiondoa mashine na haihitaji kukaa muda mrefu sana kama unavyovuna asali”anabainisha Kitosi

Mfumo ni rafiki kwa utunzaji mazingira
Akizungumzia mfumo huo na utunzaji wa mazingira,Kitosi anongeza kuwa mfumo huo unamsaada mkubwa sana kwenye kilimo na utunzaji wa mazingira.
Anasema sumu ya nyuki mara nyingi inapatikana katika mikia na mara nyingi yeye hutumia kujilinda au ulinzi lakini ukiweka mashine hiyo na nyuki kutoa sumu yake itakuwa imeshaisha mwilini mwake.
“Sasa akishatoa sumu hiyo ili awe na sumu nyingine katika mkia wake basi huchukua siku moja,mbili au tatu ili irudi tena kujijenga katika mkia wake,sasa ukiweka hii mashine na kuvuna kwa siku moja utawalazimisha Nyuki kuzunguka na kula vitu mbalimbali ili kurudisha ile sumu yao ambayo wanaitumia kama silaha.
“Mlinzi hawezi kukaa bila silaha sasa ni sayansi ndogo tu,kadiri nyuki anavyozunguka kutafuta kuirudisha ile sumu yake si anakuwa anazunguka katika maua,kwenye miti na maeneo mengine mengi anakuwa anagusa polen zilizoko katika maua tofautitofauti hivyo anafanya uchavushaji ambapo ndipo mimea mbalimbali inakuwa inazaliana na kukua”anafafanuwa Kitosi
Wakati anatoa sumu hiyo mkia wake hubakia bila kukatika tofauti aking’ata kawaida ambapo mkia wake hukatika,mashine pia inakuwa na kioo baada ya nyuki kung’ata waya zilizowapiga shoti ndipo majimaji hayo yenye sumu hudondoka kwenye kioo kwa uzito wa 0.6 gram kwa kutegemea na kundi la nyuki na huchukua dakika 30 kuvuna sumu hiyo “anasema Kitosi
Sumu ya Nyuki ni dawa
Kitosi anasema hiyo ni sumu kama zilivyo dawa za hospitali na hapo itategemea umezitumiaje hivyo kuna utaalamu wa kutengeneza ili upate dawa inayotokana na sumu ya nyuki kwa matumizi mbalimbali.
“Sisi tumejikita zaidi katika kutengeneza mfumo lakini wapo wataalam ambao wakiuziwa hiyo sumu basi wao wanajua namna gani watu wa viwanda vya kutengeneza dawa mbalimbali wanavyotengeneza.
“Ukienda nchi kama Algeria,India ikiwemo China wanatumia sana teknolojia hiyo na ndiko wanakovuna sana sumu hiyo ya nyuki lakini kwa kifupi inatibu magonjwa kama misuli kukakamaa na mengine”anaeleza Kitosi

Kitosi anaongeza kuwa mfumo walioutengeneza ambao sasa uko sokoni na umeshaanza kutumika ni kwa ajili ya kuvuna sumu ya nyuki pekee lakini Kampuni yao inaendelea na utafiti kwenye mazao mengine ili kuwapelekea wakulima mifumo mingine ikiwemo kutoa elimu na vifaa.
Kitosi anabainisha kuwa tayari mfumo walioutengeneza unafanyakazi katika mikoa ya Tabora,Geita,Morogoro eneo la Ifaraka na wanaendelea kupokea taarifa mbalimbali za mafaniko ya mashine zao.
“Sisi hizi mashine tunauza 500,000 sasa kuna mwingine hana hiyo pesa ya kununua mashine kwani wakulima wengi maisha yao wanahangaika,sasa tunachotaka kufanya kuna uwezekano wa sisi kuja kukodisha mashine hizo hapo baadaye .
“Mkulima anachukua na anakodi kwa mwezi mmoja na anakwenda kuitumia na kisha anauza kwa sababu mifumo yetu ni ya kisasa upo uwezekano wa kupata taarifa zote kutoka kwa mkulima na tunaweza kujua kama mashine imetumika au haijatumika.
“Naweza nikampa mkulima bure kwamba nenda kavune lakini mimi nitajua kwamba amevuna mara 10 au kwa kiwango gani na kwa muda gani na mwisho tutaona namna ya wote tunavyoweza kufaidika anasema Kitosi.
Kitosi anaongeza kuwa kwa yule anayeweza kununua mashine basi atanunua na yule ambaye hana uwezo basi wanajaribu kuona namna ya kushirikiana nao kwa kuwaazima mashine.
Dira ya Maendeleo 2050
Akizungumzia kuhusu Dira ya Maendeleo 2050,Mhandisi Kitosi anabainisha kuwa ubunifu wao unaendana na Dira hiyo kwani mahitaji yakiwa mengi ya mashine hizo ndipo ajira zinaongezeka lakini pia ubunifu wao utasadia upatikanaji wa mashine hizo hapa nchini bila kuagiza nje ya nchi.
“Sisi tungependa kuona shughuli za ufugaji wa nyuki zinafanywa kitaalamu zaidi kwa kutumia vifaa vizuri zaidi ambavyo vinatengenezwa hapa hapa nchini ili watu wakiwa na changamoto mbalimbali waweze kurudi kwetu na mbalina kuzalisha ajira lakini pia wataongeza mapato kwa wakulima kwa kuuza sumu ya nyuki anaongeza Kitosi.
Aishukuru Serikali kumwezesha bunifu yake kuingia sokoni
Akizungumzia kuhusu kuwezeshwa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kutimiza ndoto yake ya kuongeza thamani mazao ya nyuki,Mhandisi Kitosi anafafanuwa kuwa katika hatua za awali za utafiti wa kutengeneza kifaa hicho ,Serikali iliwapatia kiasi cha Sh.Milioni 28 mwaka 2022.
“Bila juhudi za Serikali nafikiri tusingeweza kufika hapa kwa sababu utafiti ni gharama kwani unakwenda unatengeneza kinashindwa kufanya kazi unarudi,kila kitu ni gharama na unanunua vifaa.
“Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) walituwezesha kupitia Mfuko wa Sayansi Innoviation tulipewa jumla ya Sh.Milioni 22 na ndipo tulipoweza kufikia hatua hii,kwa hiyo tunaishukuru Serikali lakini pia tunayo mengi ya kufanya zaidi mbele”anabainisha Kitosi.



Discussion about this post