NA GOODLUCK HONGO
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere amebaini matukio ya uwindaji haramu kuwa yamesababisha vifo vya wanyamapori 577 huku Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ikiongoza kwa vifo 325 sawa na asilimia 56 ya vifo vyote vilivyotokea katika hifadhi.
Hayo ameyabainisha katika Ripoti Kuu ya Mwaka ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 iliyotolewa tarehe 30/3/2026
Amesema Ukaguzi wa Taarifa ya Mwaka ya Utekelezaji wa Kimkakati ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa za Tanzania ya mwaka 2024/25 iliyohusu Hifadhi za Taifa 10 yalibainika matukio 1,962 ya uwindaji haramu ambao ulisababisha vifo vya wanyamapori 577.
“Hali mbaya zaidi ilikuwa katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ambapo matukio 186 ya uwindaji haramu yalisababisha kuuwawa kwa wanyamapori 325, ikiwa ni asilimia 56 ya vifo vyote vya wanyamapori katika Hifadhi 10 za Taifa”amesema CAG Kichere
Katika ripoti hiyo CAG Kichere amebainisha kuwa Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ilikuwa na matukio ya uwindaji haramu 431 na idadi ya vifo vya wanyamapori 39 ambapo Hifadhi ya Taifa Tarangire ilikuwa na matukio ya uwindaji haramu tisa na idadi ya vifo vya wanyamapori ilikuwa ni 11.
“Hifadhi ya Taifa Saadani ilikuwa na matukio ya uwindaji haramu 109 na idadi ya vifo vya wanyamapori 56, Hifadhi ya Taifa Mikumi ilikuwa na matukio ya uwindaji haramu 87 na idadi ya vifo vya wanyamapori 21.
“Hifadhi ya Taifa Ruaha ilikuwa na matukio ya uwindaji haramu 436 na idadi ya vifo vya wanyamapori 50 ,Hifadhi ya Taifa SerengetI ilikuwa na matukio ya uwindaji haramu 86 na idadi ya vifo vya wanyamapori 325.
“Hifadhi ya Taifa Katavi ilikuwa na matukio ya uwindaji haramu 135 na idadi ya vifo vya wanyamapori 0,Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara ilikuwa na matukio ya uwindaji haramu 77 na idadi ya vifo vya wanyamapori 0 na Hifadhi ya Taifa Arusha ilikuwa na matukio ya uwindaji haramu 44 na idadi ya vifo vya wanyapori 10”amefafanuwa CAG Kichere
CAG Kichere amebainisha kuwa jumla ya matukio ya uwindaji haramu ni 1,962 na idadi ya vifo vya wanyamapori ni 577.
Hata hivyo CAG Kichere hajataja aina ya wanyamapori waliouawa katika hifadhi hizo.

Discussion about this post