NA MWANDISHI WETU
RAIS Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete amekutana na msichana Catherine Minja aliyefanyiwa upasuaji wa moyo kwa mafanikio akiwa na umri wa miaka minne katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) miaka 18 iliyopita.
Rais Mstaafu Kikwete amekutana na Minja Mei 29,2026 jijini Dar es Salaam ambaye sasa ameshakuwa msichana mkubwa ambapo alifanyiwa upasuaji wakati huo madaktari Bingwa wa Moyo wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI) walikuwa wakitumia majengo ya MOI kabla jengo lao halijakamilika.
Rais Mstaafu Kikwete na Catherine Minja walikutana kwa mara ya kwanza Mara ya Novemba 14, 2008 wakati Dkt. Kikwete akiwa Rais alipokwenda kumjulia hali Catherine hapo MOI baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo mapema wiki hiyo.
Wakati huo Catherine alikuwa mmoja wa wagonjwa wa mwanzo kufanyiwa upasuaji huo katika taasisi hiyo.
Miaka 18 baadaye, Minja amekua na sasa ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Udaktari katika Chuo Kikuu cha Kairuki jijini Dar es Salaam.
Minja alifika ofisini kwa Rais Mstaafu Kikwete kumsalimia na kumshukuru kwa mchango wake katika kuanzisha na kuimarisha huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo nchini.
Dkt. Kikwete amempongeza Minja kwa kutimiza ndoto yake ya kusomea udaktari, jambo ambalo aliahidi kulifanya alipokuwa mtoto.
Amesema amefurahishwa kumuona akiwa mwenye afya njema na akijiandaa kulitumikia taifa kupitia taaluma ya tiba.
Kwa upande wake, Minja amesema anatamani kuwa Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo ili kuwasaidia wagonjwa wenye changamoto kama aliyowahi kupitia yeye mwenyewe, akieleza kuwa hiyo itakuwa ni moja ya njia ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha na afya njema

Discussion about this post