SERIKALI imewaonya wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini kuwa haitaongeza muda kwa yeyote atakayechelewa kukamilisha ndani ya muda uliopangwa kwa mujibu wa mkataba.
Onyo hilo limetolewa na Waziri wa Nishati Dkt.Merdad Kalemani wakati akizindua Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili, katika Kijiji cha Matiri wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.
Amesema asilimia 10 ya malipo kwa mkandarasi yatakakwa kwa kuchelewesha kazi husika.
Hata hivyo Dkt.Kalemani ameongeza kuwa ni marufuku kwa wakandarasi wanaotekeleza Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini katika maeneo yote nchini kuacha tabia ya kuhamisha nguzo za umeme zilizosimikwa
Ameeleza kuwa, mkandarasi yeyote aliyesimika nguzo, haruhusiwi kuondoa nguzo hizo na kupeleka sehemu nyingine badala yake ahakikishe anasambaza umeme katika eneo hilo na kuunga wateja wa eneo hilo
Aidha amebainisha kuwa wananchi wanafahamu serikali imetoa fedha nyingi kuhakikisha vijiji vyote vinapata umeme bila kurukwa.
“Sitaki kuona mkandarasi anafikisha nguzo ‘Site’ anazisimika, au mwingine amezirundika hapo baada ya muda anazitoa wakati hapo hakuna umeme anapeleka sehemu nyingine ni marufuku, huku ni kugombanisha serikali na wananchi wake”amesema Dkt.Kalemani

Akizungumzia Usambazaji wa Umeme katika Wilaya ya Mbinga, Dkt. Kalemani amebainisha kuwa wilaya hiyo inajumla ya Vijiji 169, kati ya hivyo 71 vimepatiwa umeme na 98 vitapatiwa umeme katika mradi huo wa REA III mzunguko wa pili kwa gharama ya Sh.Bilioni 14.34.
Mkoa wa Ruvuma una jumla ya Vijiji 554 ambapo vijiji 289 tayari vimepata umeme na 265 bado havijafikiwa katika Wilaya za Songea , Mbinga, Nyasa,Tunduru na Namtumbo ambapo zitatumika kiasi cha Sh.Bilioni 71.95 kwa mkoa mzima kukamilisha.
Discussion about this post