MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imesema Chatu ndiyo nyoka pekee asiye na sumu mwenye uwezo wa kuishi miaka 20 hadi 25.
Hayo yameelezwa leo mkoani Dar es Salaam na Ofisa Utalii wa TAWA Gregory Kalokole wakati akizungumza na wananchi waliotembelea Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika Maonyesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba yenye kauli mbiu ‘ Uchumu wa Viwanda kwa Ajira na Biashara Endelevu’ kujionea wanyama mbalimbali wakiwemo Simba,Chui,Fisi,Mamba na aina ya ndege wakubwa wakiwemo Tai.
Amesema kuna wa nyoka wa aina nyingi lakini Chatu hukua na kufikia urefu wa mita tatu hadi nne na uzito wa kilo 44 hadi 55 ambapo hupendelea kuishi katika ,maeneo yenye vichaka,nyasi ndefu na fupi,miamba na misitu.
Amefafanua kuwa chatu huwa na tabia ya kujiviringisha hata akiwa juu ya mti lakini wa kike hujiviringisha katika maeneo aliyotaga mayai ili kuyalinda na huchukua siku 90 kujiangua na watoto kutoka.
“Kuna nyoka wengi sana lakini Chatu ndiye aina ya nyoka pekee asiye na sumu na mawindo yake ni katika maeneo yenye vichaka na hupendelea kula Panya ,Swala,Tumbili,Mbwa na wengine wa jamii hizo na baada ya kuwakamata hubana na kuvunja na kisha kutoa mate yenye utelezi ili aweze kumeza kwa urahisi.”amesema Kalokole
Kalokole ameongeza kuwa Chatu hupendelea wanyama wenye damu joto na baada ya kumeza chakula chake hukaa eneo hilo hadi kitakapooza tumboni ambapo hutegemea na aina ya mnyama aliyemmeza na ikiwa ana pembe kichwa hukiacha nje.
“Adui mkubwa wa Chatu ni ndege wakubwa kama Tai na binadamu na kwamba anapatikana katika maeneo yote ya Tanzania hata kwenye makazi ya binadamu ikiwa tu kuna vyakula vyake na mazingira ya vichaka na misitu”amesema Kalokole.
Kalokole amefafanua kuwa TAWA inasimamia wanyamapori wote walioko nje ya Hifadhi za Taifa na Ngorongoro na katika maeneosho hayo ya Sabasaba wamepeleka pia wanyama wengine wakiwemo Simba na Chui hivyo ni fursa kwa watanzania kutembelea eneo hilo kujifunza.
“Wanyama wengine kama Chui huwa na tabia tofauti ambapo wengine hupendelea kukaa peke yao na ndio maana huyu tuliyemleta hapa ni aina hiyo wanaopenda kuishi peke yao”amesema Kalokole
Discussion about this post