MFUKO wa Misitu Tanzania umewezesha miradi zaidi ya 500 nchini ili kuboresha uhifadhi na usimamizi wa rasilimali misitu, ardhi na mifumo ya ikolojia kwa kutoa ruzuku.
Ruzuku hizo ambazo hutolewa kwa wadau wote wanaojihushisha na usimamizi wa rasilimali za misitu na uboreshaji wa hali ya maisha ya wananchi waishio pembezoni mwa misitu.
Hayo yameelezwa leo mkoani Dar es Salaam katika Maonyesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba yenye kauli mbiu ‘ Uchumu wa Viwanda kwa Ajira na Biashara Endelevu’.
Mfuko huo ulio chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ni Mfuko wa hifadhi ambao umeanzishwa kisheria kama njia endelevu ya kuwezesha uhifadhi wa rasilimali za misitu hapa nchini na kukabiliana na changamoto za usimamizi wa rasilimali za misitu hasa katika utekelezaji wa Sera na Sheria ya Misitu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo Mfuko huo hutoa ruzuku za aina tatu ambazo zinatofautishwa na kiasi cha fedha kitolewacho,walengwa na muda wa utekelezaji wa miradi.
Ruzuku hizo ni pamoja na ruzuku ndogo za kiasi cha fedha kisichozidi Sh.Milioni tano kinachotolewa kwa watu binafsi na vikundi ili kugharamia utekelezaji wa miradi midogo.
“Ruzuku ya kati ambayo ni kiasi kinachozidi Sh.Milioni tano na kisichozidi Sh.Milioni 20 na ruzuku kubwa ni kiasi kinachozidi Sh.Milioni 20 na kisichozidi Sh.Milioni 50 na hutolewa ili kugharamia miradi inayochukua muda mrefu”imeeleza taarifa hiyo.
Aidha imefafanua kuwa baadhi ya majukumu ya mfuko ni kutoa ruzuku kwa wadau wa misitu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya uhifadhi na uendelezaji wa misitu katika maeneo ya usimamizi yaliyopo nje ya maeneo ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Hata hivyo taarifa hiyo imebainisha matatizo yanayoukabili Mfuko huo kuwa ni pamoja na kukabiliwa na uhaba wa fedha kulingana na matarajio ya wadau ambapo kwa sasa chanzo cha mapato ya Mfuko ni serikali kutoka kwenye vyanzo vilivyoainishwa kwenye Sheria ya Misitu ya Mwaka 2002.
Taarifa hiyo imewataja wadau wa Mfuko huo ni pamoja na Jamii,Asasi za Kijamii,watafiti na Taasisi za Utafiti,wanamazingira,Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Wadau wengine ni pamoja na Taasisi za mafunzo ya misitu na nyuki,Wizara ya Maliasili na Utalii,Serikali za Mitaa zikiwemo Halmashauri za Wilaya,Taasisi zisizo za kiserikali (NGOs) na Asasi za kiraia.
Discussion about this post