MAHAKAMA ya Tanzania iko katika mpango wa kupelekea huduma ya Mahakama Inayotembea katika mikoa mingine kwa awamu ili kuwapunguzia kero wananchi.
Mahakama Inayotembea (Mobile Court Services) ambayo ni maarufu kama “Mahakama mtaani kwako”hutoa huduma zake kwa kutumia gari ambalo lina vifaa vyote kama ilivyo mahakama nyingine.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msajili Mkuu,Mahakama Tanzania leo katika maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Saba-saba imeeleza kuwa hadi sasa Mahakama hiyo inayotembea hutoa huduma zake katika mikoa miwili ya Mwanza na Dar es Salaam.
Taarifa hiyo imesema lengo la kuanzisha Mahakama Inayotembea ni kusogeza huduma za kimahakama karibu zaidi na wananchi na kuwapunguzia wananchi gharama za kufuata huduma za kimahakama.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa katika Mkoa wa Dar es Salaam maeneo ambayo Mahakama hiyo hutoa huduma zake ni pamoja na Kinondoni eneo la Bunju A katika viwanja vya ofisi ya Kata siku ya Jumatatu.
Katika Wilaya ya Ubungo hutolea huduma zake eneo la Kibamba katika Viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Ubungo siku ya Jumanne ambapo Temeke hutolea huduma zake katika eneo la Mtoni Saba-saba katika Uwanja wa Sifa siku ya Jumatano na siku ya Alhamisi hutolea huduma zake katika Wilaya ya Ilala eneo Chanika katika Viwanja vya Kata ya Chanika.
Kwa upande wa Mkoa wa Mwanza hutolea huduma zake Ilemela eneo la Buswelu katika viwanya vya soko siku ya Jumatatu ambapo kwa upande wa Wilaya ya Nyamagana hutolea huduma zake Igoma karibu na viwanja vya Ofisi ya Mtaa wa Igoma siku ya Jumanne.
“Nyamagana eneo la Igoma karibu na Ofisi ya Mtaa Igoma siku ya Jumatano,Nyamagana eneo la Buhongwa Mkolani karibu na Chuo Huria siku ya Alhamisi na Nyamagana eneo la Buhongwa karibu na Soko la Buhongwa siku ya Ijumaa.
“Gari hili lina nyenzo zote za kimahakama kama vile sehemu ya kusikilizia mashauri,kivuli na viti vya kupumzikia wateja,mlango kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum pamoja na vitendea kazi vya kisasa vinavyotumia TEHAMA ka vile kompyuta ‘printer’,runinga,kamera na mfumo wa matangazo”imefafanua taarifa hiyo.
Hata hivyo taarifa hiyo imebainisha baadhi ya manufaa ya Mahakama hiyo kuwa ni pamoja na kuondoa mlundikano wa mashauri mahakamani,kuwapunguzia gharama wananchi,kutoa haki kwa wakati,kuwapunguzia wananchi muda wa kuendesha mashauri mahakamani,
“Manufaa mengine ni kuimarisha ustawi wa jamii na kuimarisha amani na mshikamano katika jamii”imeongeza taarifa hiyo
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mhusika yeyote katika shauri asiyeridhika na uamuzi wa Mahakama Inayotembea ana haki ya kukata rufaa katika makahama ya juu.
“Utekelezaji wa maamuzi ya Mahakama Inayotembea unafanyika Mahakama za kawaida katika eneo/mamlaka husika,mfano hukumu inayotolewa na Mahakama Inayotembea katika Kituo cha Bunju,utekelezaji wake unafanyika katika Mhakama ya Mwanzo- Kawe”imefafanua taarifa hiyo.
Discussion about this post