SHIRIKA la Umeme nchini (TANESCO) limesema kukamilika kwa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere kwa kutumia maji ya Mto Rufiji(JNHPP ) utalefa faida nyingi ikiwemo nchi kuwa na umeme wa zaida na kuondoa mafuriko.
Mradi huo unaotarajiwa kukamilika Juni 14,2022 utazalisha megawati 2115 za umeme ambapo hadi kufikia mwezi mei 2021 ulikuwa umefikia asilimia 52 ya ujenzi wake.
Akizungumza leo mkoani Dar es Salaam katika Maonyesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba yenye kauli mbiu ‘ Uchumu wa Viwanda kwa Ajira na Biashara Endelevu’Mhandishi wa TANESCO Mwanji Mhaka amesema ujenzi wa bwawa hilo una faida nyingi ikiwemo kuondoa tatizo la mafuriko katika baadhi ya vijiji vilivyokuwa vikikumbwa na tatizo hilo.
Amesema hadi kufikia Juni 2022 bwawa hilo litakuwa na mita za ujazo Bilioni 32.3 ili kuanza kuzalisha umeme hivyo maji ya Mto Rufiji yatakuwa katika mtiririko maalum ambao utasaidia kuondoa tatizo la mafuriko katika baadhi ya maeneo kama Ikwiriri,Mtanza na Mloka.
Amesema mbali na kuondoa mafuriko lakini pia kutakuwa na kilimo cha umwagiliaji katika ukubwa wa heka 200,000 ambapo wakulima watafaidika na mradi huo.
“Kutakuwa na uvuvi na ufugaji na wanyama wengi watapata maji na hawatasafiri umbali mrefu sana ,kushuka kwa bei za umeme na kuwa na umeme wa uhakika pamoja na utalii ambapo wanyama wengi watazunguka bwawa.
“Itavutia wawekezaji kwa kuwa na umeme wa uhakika na ndani ya bwawa kutakuwa na visiwa ambapo pia kunaweza kujengwa hoteli za kitalii kutokana na kwamba bwawa hilo litakuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 55,000.”amesema Mhaka
Mhandisi Mhaka ameongeza kuwa kushuka kwa bei ya umeme kutachochea zaidi wananchi kutumia nishati hiyo na kuachana na matumizi ya kuni hivyo kulinda mazingira.
“Mahitaji ya umeme nchi nzima ni megawati 1,300 na uzalishaji katika vyanzo vyote ni megawati 1601 na Julius Nyerere litazalisha megawati 2115 kwa maana hiyo tutakuwa na umeme mwingi wa ziada hali itakayoongeza ukuaji wa uchumi”amesema Mhaka
Hata hivyo Mhaka amebainisha kuwa kuna miradi mingine ya kijamii itajengwa katika vijiji vilivyopo karibu na bwawa hilo mara tu uzalishaji wa umeme utakapokuwa unaendelea.
Discussion about this post