CHUO Kikuu cha Mzumbe wameweka mifumo ya kutoa mafunzo mbalimbali ili kuwasaidia vijana kuweza kujiari pindi wanapomaliza masomo yao
Chuo hicho kina kituo cha Uwatamizi na Malezi ya vijana ili kujifunza vitu mbalimbali ambapo zaidi ya vijana 20 wameshajiari.
Hilo limejitokeza juzi,katika banda la chuo hicho katika Maonyesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba yenye kauli mbiu ‘ Uchumu wa Viwanda kwa Ajira na Biashara Endelevu’.
Mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho wa Shahada ya Sayansi ya Uzamili katika Mipango na Menejimenti ya Miradi Kampas ya Morogoro Nelson Kisanga amesema
wapo katika kituo cha Uwatamizi na Malezi ya vijana chuoni hapo kujifunza vitu mbalimbali.
Amesema kupitia kituo hicho wametengeneza mfumo wa Aquaponics ambao unajumuisha ufugaji wa samaki na kilimo cha mboga mboga.
Kisanga amesema wametengeneza mfumo huo ambao chini wanafuga samaki na juu wanafanya kilimo cha mbogamboga lengo likiwa ni kukabiliana na changamoto ya ajira.
Kisanga ameongeza kuwa mbali na mfumo huo lakini pia wanabadilisha taka na kuwa wadudu kwa ajili ya chakula cha mifugo kama vile kuku, Nguruwe na hata samaki.
“Tunafanya vitu vingi pia kituo hiki kimetusaidia vijana kufika mbali kwani tayari tumeshasajili kampuni yetu ya Real Agriculture Group,” amesema Kisanga.
Ameongeza kuwa kupitia kituo hicho wameweza kuongeza mnyororo wa thamani kwa kukuchakata viazi lishe na kupata unga kwa ajili ya kutengeneza juisi, chapati na mikate.
Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo hicho Kampas ya Morogoro Dkt. Bahati Ilembo, amesema Chuo Kikuu cha Mzumbe kinatoa program nyingi za ujasiriamali na kwamba kituo cha Uwatamizi kinahusika kukuza vipaji vya vijana.
” Tunakuza vipaji vyao kwa kukusanya mawazo yao na ubunifu wanapokuwa katika kituo hiki wanajengwa na kuongezwa uwezo ili mawazo yao ya ubunifu yaweze kuwasaidia,” amesema.
Mhadhiri huyo ameeleza kuwa wana vijana takribani 50 ambao wameweza kuendelezwa kati yao 20 tayari wanajitegemea kwa kutengeneza bidhaa zao na kuuza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chuo hicho Rose Joseph ameeleza kuwa wana mfumo uliowekwa kwenye masomo ya kibiashara, teknolojia na ubunifu ambao unaendana na kauli mbiu ya mwaka huu katika Maonyesho hayo.
” Kwa misingi ya kuunga mkono serikali katika kuinua uchumi na kufikia wa kati. Tuna changamoto kubwa ya ajira vijana wanamaliza vyuo vikuu wanabaki kuzurura mitaani na karatasi kutafuta kazi “amesema Joseph
Joseph amefafanua kuwa Chuo cha Mzumbe kimelenga kumsaidia kijana kuondokana dhana ya kuajiriwa baada ya kumaliza masomo yake kwa kumjengea uwezo wa kubuni vitu ili wanapomaliza wawe na miradi mikubwa na kuweza kuajiri vijana wengine.
Discussion about this post