MKUU wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla amesema Fukwe zote za Mkoa huo yakiwemo maeneo ya wazi zitaboreshwa na kuwa sehemu ya utalii.
Makalla amesema amefanikiwa kupata wadau waliokubali kuwajengea wafanyabiashara wa ufukwe wa Coco vibanda vya kisasa na kuboresha mandhari ya ufukwe huo ili uwe kwenye mwonekano wa Kisasa.
Makalla ametoa kauli hiyo leo Agosti 24,2021 mkoani Dar es Salaam mara baada ya kutembelea ufukwe huo akiambatana na Viongozi kutoka Wilaya ya Kinondoni na wadau waliokubali kuwa sehemu ya maboresho ya fukwe hizo.
Akizungumza na wafanyabiashara wa eneo hilo Makalla amesema dhamira yake na serikali ni kuona Fukwe zote za Mkoa wa Dar es Salaam zinaboreshwa ikiwemo Coco kuwa ya kisasa na shughuli za utalii.
Makalla ameongeza kuwa ni muhimu kwa Manispaa ya Kinondoni kuanza ujenzi wa Ofisi na vyoo vya kisasa ikiwemo kupeleka umeme katika eneo lote la ufukwe huo.
Mpango wa kuboresha Fukwe za Dar es salaam unaenda sambamba na maboresho ya maeneo ya wazi, bustani za kupumzika, usafi na upandaji wa miti, maua na kingo pembezoni mwa Barabara.

Wakati huo huo Makalla amezindua mfumo wa kukusanya ushuru wa maegesho kidigitali ambapo fedha zote zitapokelewa moja kwa moja serikalini.
Amesema mfumo huo utaondoa rushwa na uonevu ambapo utaongeza ufanisi katika ongezeko la mapato.
Makalla amefafanua kuwa mfumo huo utaanza rasmi kutumika Septemba mosi mwaka huu na utaenda kutatua kero na changamoto mbalimbali zilizokuwa zinajitokeza
Discussion about this post