DARAJA jipya la Selander linalopita baharini mkoani Dar es Salaam limekamilika kwa asilimia 91 ambapo kazi iliyobaki ni kuunganisha eneo la juu pekee ili lianze kutumika.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) ambayo imeelezea hatua zilizofikiwa hadi sasa juu ya ujenzi wa daraja hilo.
“Daraja jipya la Selander limekamilika kwa asilimia 91,na wakati ujenzi wa daraja hili ukimaliziwa,kazi inayoendelea sasa ni kuunganisha eneo la juu la Daraja,miundombinu bora ya barabara ,madaraja na viwanja vya ndege ni kwa maendeleo ya Taifa”alieleza taarifa hiyo.

Darala hilo linajengwa kwa gharama ya Sh.Bilioni 243 ambalo ni la kipekee Afrika Mashariki na Kati na lilizinduliwa ujenzi wake Julai 23, 2018 na Hayati Rais Dkt.John Magufuli.
Daraja hilo ambalo ujenzi wake ukiwa ni wa miezi 36 sawa na miaka mitatu, huku likiwa na urefu wa Kilomita 6.23 ambapo kati ya hizo Kilomita 1.03 ni daraja na Kilomita 5.2 ni barabara unganishi.
Hadi kukamilika kwake litaunganisha barabara ya Barack Obama na eneo la Fukwe za Coco(Coco Beach)katika makutano ya barabara za Kenyatta na Toure.
TANROADS imekuwa Wakala bora wa Serikali kutokana na kujijengea heshima ya kusimamia kikamilifu miundombinu ya barabara na madaraja makubwa nchini hali inayoongeza thamani ya pesa za walipa kodi na kutatua kero za wananchi.

Daraja la Selander(Salenda) jijini Dar es Salaam likiwa katika hatua za kukamilika kwake ili lianze kutumika(Picha na mpigapicha wetu)
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikiendeleza miradi yote iliyoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tano ya Hayati Rais John Magufuli kwa kuhakikisha kuwa fedha zinapatikana ili kukamilisha miradi hiyo.


Discussion about this post