MKUU wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla amesema haridhishwi na kasi ndogo inayofanywa na Kampuni ya JASCO inayojenga barabara ya Makongo na kumtaka kuikabidhi barabara hiyo ifikapo Oktoba 8,2021.
Amesema Serikali imefanya kila kitu ikiwemo kulipa fidia,kuondoa miundombinu mingine ili ujenzi wa barabara hiyo ufanyike kwa haraka na bila visingizio lakini kasi ya Kampuni hiyo katika ujenzi hairidhishi.
Makalla ameyasema hayo jijini Dar es Salaam mara baada ya kutembelea eneo la Makongo ambako mradi huo wa ujenzi wa barabara unafanyika.
“Habari ya Makongo mimi sitaki tena kusikia,mimi ni mwenyeji,mimi nilikuwa Mwenyekiti wa Kata hii,naomba mradi huu wa Makongo ukamilike kwa wakati visingizio vyote hatutaki”amesema Makalla
Hata hivyo Makalla ameonyesha kuchukizwa na tabia ya mkandarasi huyo kuonekana eneo la kazi siku pekee ambayo viongozi wanatembelea barabara hiyo jambo linalosababisha kusuasua kwa mradi huo na kuleta kero na mateso kwa wananchi.
“Tayari Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA),Shirika la Umeme nchini(TANESCO) na Kampuni ya Simu nchini(TTCL) wameondoa miundombinu yao na wananchi wote wamelipwa fidia walizokuwa wakidai hivyo sioni sababu yoyote ya mkandarasi huyu kuchelewesha mradi”amesema Makalla
Barabara hiyo ya Makongo ina urefu wa Kilomita 4.5 na ujenzi wake unagharimu zaidi ya Sh. Bilioni nane ambapo ikikamilika itasaidia kurahisisha usafiri kwa wakazi wa Makongo na Goba ikiwemo kupunguza msongamano wa magari kwenye Barabara ya Bagamoyo.


Discussion about this post