ZANZIBAR imetajwa kuongoza katika ufugaji wa Samaki aina ya Mwatiko ambapo Kaya 368 zilijihusisha na ufugaji huo huku Tanzania Bara ikiongoza kwa ufugaji wa Sato wakiwemo Kambale.
Hata hivyo uzalishaji wa samaki ulikuwa tani 12,936 ambapo kwa Tanzania Bara ulikuwa tani 12,873 na tani 64 kwa Tanzania Zanzibar na kati ya hizo, tani 12,626 zilitoka kwa wafugaji wadogo na tani 310 kutoka mashamba makubwa.
Hayo ni kwa mujibu wa Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Mwaka wa Kilimo 2019/20 katika Ripoti ya Matokeo Muhimu kwa Sekta za mazao,mifugo na ufugaji wa samaki iliyotolewa Agosti mwaka huu na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Ripoti hiyo ya NBS imebainisha kuwa matokeo ya Sensa hiyo yameonesha kuwa ufugaji wa samaki ulifanywa na wakulima wadogo na mashamba makubwa.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa jumla ya kaya 26,662 zilijihusisha na ufugaji wa samaki wa aina mbalimbali ambapo kati ya hizo, kaya 26,294 ni za Tanzania Bara na kaya 368 ni za Tanzania Zanzibar.
Hata hivyo idadi ya mashamba makubwa yanayofuga samaki yalikuwa 78, kati ya hayo mashamba makubwa 63 ni kwa Tanzania Bara na mashamba 15 ni ya Tanzania Zanzibar.
“Samaki aina ya Sato walifugwa na wakulima wengi Tanzania Bara ambapo Kaya 21,704 na mashamba makubwa yakifikia 52 ikilinganishwa na aina nyingine za samaki ambapo Kaya 8,189 na mashamba makubwa 41 .
“Kwa upande mwingine, Mwatiko ndiyo aina pekee ya samaki waliofugwa Tanzania Zanzibar na kaya 368 na mashamba makubwa 15”imefafanua ripoti hiyo
Kwa upande mwingine ripoti hiyo imefafanua kuwa wafugaji wadogo wanaofanya Kilimo cha Samaki wameongezeka kutoka 10,794 kwa mwaka 2007/08 hadi 26,662 mwaka 2019/20 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 100.
Mbali na hilo lakini pia jumla ya vifaranga vya samaki 49,379,641 vikiwemo 49,206,355 kwa Tanzania Bara na 173,286 Tanzania Zanzibar vilipandikizwa na wakulima wadogo, wakati mashamba makubwa yalipandikiza vifaranga 3,599,969 vikiwemo 3,442,578 kwa Tanzania Bara na 157,391 kwa Tanzania Zanzibar
“Ujumbe Muhimu,matokeo yanaonesha kuwa, idadi ya kaya zinazojihusisha na ufugaji samaki zimeongezeka kutoka kaya 10,794 Mwaka 2007/08 hadi kaya 26,662 Mwaka 2019/20.
“Ongezeko kubwa la idadi ya kaya zinazofuga samaki linatoa fursa ya uwekezaji wa viwanda vya kuzalisha vyakula kwa ajili ya samaki wafugwao.
“Vyakula hivyo kwa sasa huagizwa kutoka nje ya nchi na hivyo kuongeza gharama za uzalishaji ”imeeleza ripoti hiyo.
Discussion about this post