MAMIA ya watu katika Jimbo la Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wamepatwa na ugonjwa wa kuhara ikiwemo kutokwa na vipele baada ya kutumia maji ya Mto Kasai yanayodaiwa kuwa na sumu.
Hata hivyo watu hao pia wanadaiwa kula samaki waliokufa kutokana na sumu hiyo iliyosambaa katika Mto Kasai ambao unapita katika jimbo hilo.
Maafisa wa serikali katika Jimbo la Kasai wamesema kuwa, maji ya mto mkoani humo yalibadilika rangi ambapo viboko na samaki waliokufa walikutwa kwenye maji hayo wakielea.
Sumu hiyo inadaiwa kutoka eneo la uchimbaji wa Almasi nchini Angola ambapo iliripotiwa kutoa kemikali za sumu tangu mwezi Julai mwaka huu ambazo zimechafua maji katika mito ya Kasai na Tshikapa nchini DRC.
Naibu Waziri Mkuu anayeshugulikia Mazingira wa Eve Bazaiba amewaambia waandishi wa habari baada ya kulitembelea eneo lililoathirika kwamba zaidi ya kesi 4000 za kuhara zimesajiliwa katika maeneo 13 kati ya 18 yaliyoathiriwa katika jimbo la Kasai.
Bazaiba ameongeza kuwa, wakazi wa maeneo yaliyoathirika wajiepushe na kula samaki waliokufa na matumizi ya maji ya mito hiyo
Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Kasai wameeleza kuwa, wamepatwa na vijiupele mwilini baada ya kutumia maji hayo machafu.
Tayari serikali ya Kinshasa imechukua hatua za kuhakikisha kuwa, maji safi yanapelekwa katika maeneo yaliyoathirika.
Hofu imetanda katika Mto Kongo ambao ni wa pili kwa urefu barani Afrika ukitanguliwa na Mto Nile kwamba nao pia unaweza kukumbwa na hali hiyo kutokana na Mto Kasai kuingiliana na mto huo.
Discussion about this post