SERIKALI kupitia Sekta ya Uvuvi imeingia makubaliano na Chuo Kikuu cha Nelson Mandela pamoja na Mfuko Kichocheo wa Kilimo Tanzania (TACT) ili kujenga Kituo cha Ubunifu katika Uvuvi na tasnia ya Ukuzaji Viumbe Maji.
Lengo la ujenzi huo ni kusaidia kutatua changamoto za utafiti, ugani na ubunifu ili kuongeza tija katika Sekta hiyo nchini.
Akizungumza wakati wa utiaji saini katika mkataba wa makubaliano hayo mwishoni mwa wiki mkoani Kagera,Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayesimamia Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah amesema kuwa kuanzishwa kwa Kituo hicho kutasaidia kutatua changamoto nyingi zinazokabili sekta ya Uvuvi na tasnia ya Ukuzaji Viumbe Maji.
“Napenda kuwaahidi wadau wote wa Sekta ya Uvuvi kuwa Wizara itaendelea kuunga mkono juhudi za wavuvi, Wakuzaji Viumbe Maji, Wachakataji, na Wafanyabiashara wa bidhaa za Uvuvi ili ziweze kuwa na tija na kuleta ustawi wa wadau wote nchini,” amesema Dkt. Tamatamah
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji, Mfuko Kichocheo wa Kilimo Tanzania, Dkt. John Kyaruzi amesema wameamua kuwekeza katika utafiti kwenye Sekta ya Uvuvi ili iweze kuwa endelevu na kuwasaidia wawekezaji kuwa na taarifa za msingi zitakazowasaidia kuwekeza kwa tija ili kuimarisha biashara zao.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali, Charles Mbuge amewataka Viongozi wa Mkoa huo kuupokea mradi huo kwa kuwa hiyo ni neema iliyowafikia katika eneo lao.
Amesema kuwa viongozi hao hawana budi kukusimamia mradi huo unafanikiwa ili uweze kuleta tija kwa jamii hususani vijana ili waweze kujiajiri kupitia shughuli za uvuvi na kukuza uchumi wao na wa nchi pia.
“Halmashauri zetu mpo hapa pamoja na Viongozi, naomba suala hili mlitilie maanani, uwekezaji huu ukifanikiwa hapa kwetu utasaidia kujenga uchumi wa Mwananchi mmoja mmoja hadi Taifa kwa ujumla,” amesema Meja Jenerali Mbuge
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Nelson Mandela, Prof. Emmanuel Luoga amebainisha kuwa nia ya Chuo hicho ni kufanya tafiti zitakazotoa matokeo chanya kiuchumi na kiikolojia ili kufanya shughuli za uvuvi kuwa endelevu.

Katika sehemu ya makubaliano hayo Wizara imepanga kufanya tathmini ya mazingira na kurekebisha sera na sheria zote ambazo kwa namna moja au nyingine zimekuwa kikwazo kwa shughuli za uvuvi.
Chuo Cha Nelson Mandela kitajikita kufanya tafiti tumizi ili kusaidia Sekta ya Uvuvi na wadau wake kuwa na taarifa sahihi zitazowasaidia kuboresha shughuli zao na Mfuko Kichocheo wa Kilimo (TACT) watawekeza mitaji ili kuchachua uwekezaji katika Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji nchini.
Discussion about this post