MKUU wa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, Mhandisi Richard Ruyango amewaagiza Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru kutenga siku ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi wilayani humo.
Ruyango ameyasema hayo wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kilichokutana mwishoni mwa wiki iliyopita huku madiwani wakiwasilisha taarifa za Kata zao katika kipindi cha Aprili hadi June 2021.
Mhandisi Ruyango amesema ni muhimu kwa viongozi wa ngazi zote katika wilayani humo kuwa na siku moja kwa ajili ya kusikiliza matatizo ya wananchi ambapo wengine yanaweza kutatuliwa bila kufikishwa ngazi za juu zaidi hivyo kupunguza kero zo.
“Viongozi kuanzia ngazi za Kitongoji, Vijiji, Kata na Wilaya kutenga siku ya Jumanne kusikiliza na kutatua kero za wananchi .
“Si vyema mwananchi ana kero ambayo inaweza kutatuliwa na Viongozi wa eneo lake, atumie nauli na muda wake kuja ngazi za Wilaya” amesema Ruyango
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru Zainabu Makwinya amesema ni muhimu kwa Watumishi wote wa Halmashauri hiyo kusikiliza kero za wananchi kwa wakati sambamba na kutoa sababu za msingi kwa kero ambazo zinazohitaji muda.
“Maafisa Utumishi wa ngazi za Vijiji na Kata wanatakiwa kufanya uchunguzi na kutoa takwimu sahihi za wanafunzi ambao hawajaripoti shule”amesema Makwinya
Amesema kuwa maafisa Utumishi wanapaswa kufuatilia kwa karibu zaidi na kutoa taarifa sahihi kwa Maafisa Elimu kuhusu idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari na wale ambao hawajaripoti.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Jeremiah Kishili amesema mbali na changamoto nyingine zilizopo katika Sekta ya Elimu ni muhimu kuwepo na utaratibu ambao utasaidia Walimu wanaopangiwa kazi katika shule za vijijini kutopata uhamisho.
Amefafanua kuwa Walimu wasipate uhamisho usiokuwa na sababu za msingi kwa kuwa shule za vijijini zinazokabiliwa na upungufu wa Walimu.
Kishili ambaye ni Diwani wa Kata ya Imabaeny ameongeza kuwa Walimu wengi wanapopangiwa kufanya kazi katika shule za vijijini wamekuwa wakihama muda mfupi baada ya kuripoti kutokana na changamoto ndogo ndogo za kimazingira.
Amebainisha kuwa hali hiyo ya walimu kuhama inachangia wanafunzi kushindwa kufanya vizuri katika masomo yao.
Naye Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri hiyo Anjela Urassa amesema tayari wamekwishaandaa ripoti ya wanafunzi ambao hawajaripoti shule.
Amesema ni muhimu pia kwa Viongozi wa Vijiji na Kata kuelewa zaidi na kufahamu makazi ya wazazi wa wanafunzi na mazingira waliopo watoto hao ili kisaidia ufumbuzi wake.

Discussion about this post