IDADI ya watu wanaopoteza maisha kila mwaka kutokana na athari zinazosababishwa na kuumwa na nyoka wenye sumu imefikia zaidi ya 137,000 huku wengine wakipata ulemavu.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) wakati wa uzinduzi wa jukwaa maalum mtandaoni kwa lengo la kutoa taarifa na kuelimisha umma kuhusu hatari ya kuumwa na nyoka wenye sumu na nyoka wapi waliko nyoka hao hatari zaidi duniani mjini Geneva,Uswisi.
Shirika hilo limesema watu 81,000 hadi 137,000 hufariki dunia kutokana na athari zinazosababishwa na kuumwa na nyoka wenye sumu ingawa idadi kamili ya walioumwa na nyoka hadi sasa haijulikani.
Hata hivyo kwa mujibu wa WHO makadirio yanaonesha kuwa takriban watu Milioni 5.4 huumwa na nyoka kila mwaka huku Milioni 2.7 kati yao huumwa na nyoka wenye sumu kali ambao husababisha athari mbaya kwa mamilioni ya maisha ya watu na wengi wao wakiwa masikini.
Mbali ya vifo vya watu 137,000 kila mwaka, kuumwa na nyoka pia kumewaacha mamilioni ya watu na ulemavu wa maisha
WHO imebainisha kuwa kuumwa na nyoka mwenye sumu kali kunaweza kusababisha kupooza ambako kunaweza kumzuia mtu kupumua, kumsababishia maradhi ya kutokwa na damu, matatizo ya figo yasiyoweza kutibika na kuharibu mishipa ambayo inapelekea ulemavu wa maisha na kukatwa viungo.
Shirika hilo limeongeza kuwa kuumwa na nyoka ni moja ya magonjwa yaliyopuuzwa NTDs ambayo athari zake ni kubwa na mbaya kuliko inavyodhaniwa.
WHO imebainisha kuwa waathirika wakubwa ni watu wanaofanya kazi katika Sekta ya Kilimo na Watoto huku maeneo yaliyoathirika na kuwa hatarini zaidi ni Afrika, Asia na Amerika ya Kusini katika maeneo ya Vijijini
“Mathalani barani Asia watu wapatao milioni 2 hudhurika na sumu ya nyoka kila mwaka na Afrika watu 435,000 hadi 580,000 huhitaji matibabu kila mwaka baada ya kuumwa na nyoka.
“Ili kupunguza idadi ya vifo na ulemavu utokanao na kuumwa na nyoka ni lazima kuziwezesha na kuzishirikisha jamii, pili kuhakikisha kuna matibabu salama na yenye ufanisi, tatu kuimarisha mifumo ya afya na nne kuongeza ushirika, uratibu na rasilimali za kupambana na zahma hii”imefafanua taarifa hiyo.

Discussion about this post