SERIKALI imeitaka jamii nchini kuacha kuwaficha na badala yake kuwafichua watoto wenye ulemavu wa kusikia (Viziwi)kwa kuwa wana haki ya kupata elimu sawa na watoto wengine wasiona na ulemavu
Mbali na ulemavu huo lakini pia watoto hao wana uwezo wa kufanya vizuri hata zaidi ya watoto ambao hawana ulemavu wa kusikia.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Arusha na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Walemavu Ummy Nderiananga katika mahafali ya kwanza ya kidato cha nne katika Shule ya Wanafunzi wenye Ulemavu wa Kusikia ya Shirika la Roho Mtakatifu na mahafali ya 14 ya Shule Sekondari ya Wavulana Tengeru.
Amesema kuwa jamii inapaswa kuachana na dhana ya kuwaficha nyumbani watoto wenye ulemavu wa kusikia badala Yake wawafichue na kuwapeleka shuleni kwa kuwa nao wana haki ya kupatiwa elimu bora kama walivyo watoto wengine kwenye jamii.
Hata hivyo Nderinanga amefurahishwa na jitihada nzuri zinazofanywa na watoto wenye ulemavu wa kusikia(viziwi) katika elimu ambapo wengi wameonesha kufanya vizuri.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shule ya wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia Padri John Asei ameiomba serikali kuwa na mitaala ambayo inahusisha watoto wenye ulemavu kuanzia elimu ya awali mpaka chuo kikuu ili kuwawezesha kupata elimu bora.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Tengeru Mwalimu Gaudens Mtui amesema kuwa shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri kutokana na maadili mema ambayo wamekuwa wakifundishwa kwani tangu kuanzishwa kwake hakuna mwanafunzi aliyewahi kupata ufaulu wa alama sifuri.
Hata hivyo Mtui amebainisha kwamba wanatarajia wanafunzi wa shule hizo kuweza kufanya vizuri zaidi katika mitihani ya kuhitimu kidato cha nne ikiwa na wahitimu 126 kidato cha nne huku wanafunzi wanaohitimu katika shule ya ulemavu wa kusikia wakiwa saba.


Discussion about this post