MPANGO wa Taifa wa Damu Salama nchini umezindua kampeni ya kitaifa ya kuihamasisha jamii kuchangia damu ili kuokoa vifo kwa akina mama wajawazito vinavyotokana na uzazi.
Kampeni hiyo inakuja kutokana na kile kinachoelezwa kuwa vifo vingi vya akinamama wajawazito vilisababishwa na kutokwa damu nyingi baada ya kujifungua hivyo ni jukumu la jamii yote kuchangia damu ili kuokoa vifo hivyo.
Akizungumzia Kampeni hiyo Septemba 20,2021 jijini Dar es Salaam,Mkuu wa Idara ya Ukusanyaji Damu katika Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Dk. Avelina Mgasa amesema kauli mbiu ya kampeni za mwaka huu wa 2021 ni “Changia Damu Kuokoa Wanaoleta Uhai Duniani”.
“Kampeni hii inalenga kuihamasisha jamii kujitolea kutoa damu kwa hiyari ili kuokoa maisha ya kina mama wajawazito ambao wanatumika kama chombo cha kuleta uhai duniani” amesema Dk. Mgasa

Maabara inayotumika kuhifadhia damu na kuipima kabla ya kuruhusiwa kutumika kwa ajili ya wagonjwa wanaohitaji kuongezewa damu(Picha na mpigapicha wetu)
Dk.Mgasa amefafanua kuwa Kauli mbiu inatupa hamasa na kuihamasisha jamii kujitolea kuchangia damu kwa hiari ili kuongeza upatikanaji wa damu ya kutosha na salama ambayo itasaidia kuokoa maisha ya kina mama ambao hupoteza maisha kila siku kutokana na matatizo ya uzazi na wakati wa kujifungua.
Ameongeza kuwa Kampeni hiyo iliyozinduliwa katika Kanda zote saba za kukusanya damu nchini imeanza siku ya Jumatatu ya Septemba 20,2021 na imelenga kukusanya chupa za damu 19,514 kutoka kwenye timu 226 zilizopo nchi nzima ambazo ni asilimia tatu ya malengo yao ya damu kwa mwaka.
Aidha Dk. Mgasa ameongeza kuwa Kampeni ya mwaka huu inailenga jamii kuwa wachangiaji wa damu kwa kuwa asilimia 80 ya damu inayokusanywa nchini, inakusanywa kutoka kwa wanafunzi na vijana wanapokuwa shule za sekondari na vyuoni.

Mkuu wa Idara ya Ukusanyaji Damu katika Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Dk. Avelina Mgasa akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) mkoani Dar es Salaam hivi karibuni jinsi Damu salama inavyohifadhiwa tayari kwa matumizi ya binadamu(Picha na mpigapicha wetu)



Discussion about this post