SERIKALI imeandaa Mpango-Kazi wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya kemikali aina ya Zebaki kwa Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu ili kulinda afya za wananchi,viumbe hai na mazingira.
Kemikali hiyo hatari inadaiwa kuharibu ubongo na mfumo wa mishipa ya fahamu, figo,kuzaliwa watoto wenye ulemavu,kupoteza kumbukumbu ikiwemo kushindwa kupumua imekuwa ikiingizwa kwa kificho ambapo watumiaji wakubwa ni wachimbaji wadogo wanayoitumia bila kufuata utaratibu wake.
Mpango-Kazi huo wa mwaka 2020-2025 umekuja ili kukidhi matakwa ya Mkataba wa MINAMATA ukiwa na lengo la kupunguza matumizi ya Zebaki ikiwezekana kuiondosha kemikali hiyo katika shughuli za wachimbaji wadogo wa dhahabu na kutumia teknolojia mbadala.
Akizungumza katika semina ya waadishi wa habari jijini Dodoma,Mkurugezi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Dk.Andrew Komba amesema Zebaki ni kemikali hatari kwa mazingira na viumbe hai na madhara yake ni ya muda mrefu.
“MINAMATA ni moja ya Jimbo lililoko nchini Japan ambalo kulikuwa na kiwanda cha kutengeneza kemikali mbalimbali na kiliajiri wakazi wengi wa eneo hilo na kemikali iliyokuwa ikitumika sana ni Zebaki.
“Maji yake yalikuwa wakimwagwa baharini na shughuli kuu katika eneo hilo ni uvuvi hivyo tangu miaka ya 1930 athari zake zinaonekana hadi sasa na mimi nilienda huko mwaka 2018 athari zake ni kubwa hivyo lazima waandishi msaidie kuelimisha umm”amesema Dk Komba
Dk Komba amefafanua kuwa serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kukabiliana na kemikali hiyo ikiwemo kutafuta teknolojia mbadala itakayoweza kutumika na wachimbaji wadogo ili kuepusha madhara makubwa kwa jamii.

Baadhi ya Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini na wachimbaji wadogo wa dhababu, wakimsikiliza Meneja wa Mgodi wa Chikoa uliopo nje kidogo ya Jiji la Dodoma Zebedayo Matunde wakati akitoa maelezo jinsi matumizi ya kemikali ya zebaki inavyotumika katika kuchenjulia madini kulingana na miongozo iliyowekwa na serikali (Picha na mpigapicha wetu)
Kwa upande wake Mhandisi Kamukuru Maganya kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira amesema Zebaki inayotumika katika shughuli za wachimbaji wadogo hapa nchini huingizwa kutoka nje ya nchi kupitia njia zisizo rasmi na huonekana katika matumizi pekee.
“Ni lazima uingizwaji,uhifadhi,matumizi yake ya Zebaki yafuate utaratibu maalum kwani hadi sasa kuna wachimbaji wadogo zaidi ya milioni 1.2 na wote hawa wanatumia kemikali ya zebaki kupata dhahabu”amesema Maganya
Kwa upande wake Abel Madaha kutoka Tume ya Madini amesema kemikali hiyo inapobaki katika ardhi hubadilika na kuwa sumu hivyo serikali iliamua kuweka Sheria na Kanuni juu ya Zebaki na kemikali nyingine ili kuweza kudhibitiwa.
“Serikali imehakikisha inajenga vituo maalum vya uchenjuaji wa dhahabu,kutoa mafunzo na semina mbalimbali kwa wachimbaji wadogo ambao ndio waathirika wakubwa katika matumizi ya kemikali hiyo na kuhakikisha kuwa wanavaa vifaa kinga wakati wa uchenjuaji wa dhahabu”amesema Madaha
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) John Chikomo amebainisha kuwa ni wajibu wa waandishi wa habari kuisaidi serikali katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa sahihi za mazingira kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Andrew Komba akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Mpango-Kazi wa Kupunguza Matumizi ya kemikali ya Zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu (2020 -2025), jijini Dodoma jana.Kushoto ni Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) John Chikomo na Ofisa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Kamukuru Maganya
Oktoba 9,2013,Serikali kutoka nchi mbalimbali duniani zilianza kutia saini Mkataba wa Kuzuia Matumizi ya Zebaki baada ya mashauriano ya miaka minne .
Mkataba huo unaweka uthibiti na upunguzaji wa matumizi ya madini hayo ya Zebaki katika vifaa tiba na kwenye sekta ya uchimbaji madini na viwanda vya saruji. Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Mazingira (UNEP) limefafanuwa kuwa madhara ya kiafya yanayotokana na matumizi ya Zebaki ni pamoja na kuharibu ubongo na mfumo wa mishipa ya fahamu




Discussion about this post