NA GOODLUCK HONGO
TANI 24 za kemikali hatari ya Zebaki hutumika kwa mwaka katika shughuli za uchenjuaji wa dhahabu nchini ambapo wachimbaji wadogo ndio watumiaji wakubwa.
Hayo yamebainishwa katika Mpango-Kazi wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki kwa Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu kwa mwaka 2020-2025 ulioandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira.
Mpango huo umekuja baada ya Jumuia ya Kimataifa mnamo mwaka 2013 kupitisha Mkataba wa MINAMATA wenye madhumuni ya kulinda afya ya binadamu dhidi ya madhara ya uchafuzi wa mazingira unaotokana na Zebaki.
Hata hivyo kutokana na serikali kuona umuhimu wa kulinda afya za watanzania na mazingira kwa ujumla iliuridhia mkataba huo na kuusaini mwaka 2020.
Mpango-Kazi huo umefafanua kuwa wachimbaji wadogo huchenjua dhababu kwa kutumia mbinu ambazo huhatarisha afya za binadamu na mazingira.
“Shughuli za wachimbaji wadogo wa dhahabu zimekuwepo nchini kwa zaidi ya miaka 100 huku tathmini ikionesha kuwa takribani tani 13.2 hadi 24.4 za Zebaki hutumika kwa mwaka katika shughuli za uchenjuaji wa dhahabu.
“Uchomaji holela wa dhahabu,uchenjuaji wa dhahabu karibu na maeneo ya makazi na vyanzo vya maji na uchenjuaji wa marudio yenye Zebaki kwa kutumia sayanadi kunakochangia zaidi uchafuzi wa mazingira”umefafanua Mpango Kazi huo.

Hata hivyo lengo la Mpango-Kazi huo ni kupunguza na pale inawezekana kuondosha matumizi ya Zebaki katika shughuli za Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu ili kulinda afya za wananchi na mazingira
Kwa mujibu wa Mpango-Kazi huo umebainisha kuwa,Shirika la Afya Duniani (WHO) limeitaja Zebaki kuwa ni miongoni mwa vyanzo 10 hatarishi kwa afya ya binadamu duniani.
Awali akizungumza na waandishi wa habari kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) kuhusu madhara ya zebaki,kwa mazingira na afya za binadamu Mratibu wa Mradi wa EHPMP kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Mhandisi Benjamin Mchwampaka amesema Zebaki ikiingia mwilini husababisha magonjwa ambayo kwa ujumla yanajulikana kama MINAMATA.
“MINAMATA huathiri Mfumo wa Neva na kusababisha magonjwa kama miguu na mikono kufa ganzi na kukosa nguvu, misuli kulegea, figo kuathirika, uono hafifu, kupoteza uwezo wa kusikia na kuongea,mimba kuharibika, kuzaa watoto wenye matatizo ya akili au wenye viungo pungufu, kupoteza kumbukumbu, kukosa usingizi kwa muda mrefu, kiharusi na hatimaye kifo”.
“Kutokana na athari hizo,MINAMATA inarithishwa kutoka kizazi hadi kizazi”amefafanua Mhandisi Mchwampaka
Mchwampaka amesema serikali inaendelea kuchukua hatua dhidi ya matumizi ya zebaki ikiwemo kupatikana kwa teknolojia mbadala ili kuchana na matumizi ya zebaki katika shughuli za uchejuaji wa dhahabu na kutoa elimu kwa wahusika ili kulinda mazingira na afya zao.
Kwa mujibu wa Mkataba wa MINAMATA unazitaka Serikali ambazo ni wanachama wa mkataba huo zitawajibika kisheria kuchukua hatua mbalimbali kushughulikia athari za Zebaki katika maisha yao yote”amesema Mchwampaka
Hatua hizo ni pamoja na kupiga marufuku madini mapya ya Zebaki,kutokomeza yaliyopo na kusimamia matumizi ya Zebaki katika uchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu,michakato ya utengenezaji na uzalishaji wa vitu vya kila siku kama vile vipodozi,balbu,betri na unga unaotumika kujaza meno.




Discussion about this post