NOVEMBA 28,2021 vyombo ,mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya nchi vilitoa taarifa ya vifo vya watu saba na wengine 24 kulazwa hospitali baada ya kudaiwa kula nyama ya Kasa huko Pemba Zanzibar.
Hata hivyo kwa Zanzibar hilo sio tukio la kwanza ambapo Januari,2012,watu wa familia moja walifariki dunia katika Kijiji cha Tumbe Wilaya ya Micheweni Pemba na wengine sita kulazwa hospitali wakiwa katika hali mbaya baada ya kudaiwa kula nyama ya kasa.
Kasa huyo alivuliwa kutoka baharini Januari 3,2012 ambapo baada ya kuchinjwa alitengezezwa na nyama yake kupelekwa nyumbani kwa ajili ya kitoweo.
Baada ya familia kula nyama hiyo, iliwachukua saa 3 kuanza kupata athari za nyama yake kwa kuugua.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, wa wakati huo Yahya Rashid Hemed alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataka wananchi waache ukaidi wa kula nyama ya kasa.
Amesema wananchi wakiendelea na ukaidi kwa maagizo yanayotolewa ndipo madhara yanapojitokeza jambo ambalo huathiri jamii.
Katika eneo la Pemba kunahitajika elimu kutoka kwa watalaamu ili kusaidia kufafanua umuhimu wa kuwalinda kasa na madhara yake kwa binadamu.

Kwa Tanzania Bara Shirika lisilo la kiserikali la Sea Sense limefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutoa elimu juu ya kulindwa kwa mazingira ya bahari na umuhimu wa kumlinda kasa na athari zake kwa binadamu pindi nyama yake ikiliwa na binadamu
Sea sense walianza kazi ya kuhamasisha kulindwa kwa mazingira ya bahari tangu miaka ya 2000 wakianzia na Wilaya ya Mafia mkoani Pwani na baadaye kuhamia katika wilaya zingine za Mkuranga na Kibiti.
Wilaya zingine ambazo Shirika hilo lilifanya kazi ya kulinda uvuliwaji wa kasa ni pamoja na Mkinga,Pangani,Tanga jiji na Muheza mkoani Tanga pamoja na Kigamboni mkoani Dar es Salaam na Kilwa Mkoa wa Lindi.
Katika maeneo hayo wananchi wengi wanaelewa madhara ya kula nyama ya Kasa hivyo kupunguza athari za kiumbe huyo anayeonekana kupendwa na jamii za watu wa mwambao wa bahari.
Shirika hilo lilifanikiwa kutengeneza mfumo wa maafisa Kasa zaidi ya 38 katika wilaya hizo ili kudhibiti uvuliwaji na ulaji wa nyama ya kasa ikiwemo mayai yake ambao wananchi kutoa taarifa za siri pindi wanapoona kavuliwa au kusambazwa kwa nyama yake.
Akizungumzia hali hiyo mkoani Dar es Salaam leo,mtaalamu wa masuala ya mazingira na viumbe wa baharini Omary Mapoy amesema kuna Kasa wa aina saba lakini Tanzania wapo wa aina tano pekee ambapo ni Kasa Kawaida,Ng’amba,Duvi,Kigome na Noa
Amesema aina mbili zilizobaki za kasa hupatikana katika nchi zenye baridi kali na huweza kukua hadi kufikia uzito wa tani moja lakini kasa sio samaki kama wetu wanavyodhani bali ni moja kati ya viumbe vinavyoishi majini na majike hutoka nchi kavu kwa ajili ya kutaga mayai na kisha kurudi baharini kuendelea na maisha yao.
“Kasa wana madhara makubwa kwa binadamu na kupelekea vifo kwa sababu wanakula majani na viumbe wenye sumu kama washawasha au viwavi wa baharini (jerry fish) hivyo kuwafanya kuwa na sumu.
“Faida kubwa ya uwepo kwa kasa ni chanzo cha kuongezeka kwa samaki baharini kwa sababu ile mimea na wanyama wenye sumu ikiongezeka samaki hukimbia hivyo uwepo wa kasa baharini husaidia kuongezeka kwa samaki”amesema Mapoy
Mapoy amefafanua kuwa hata binadamu akiguswa na viwavi hao (jerry fish) huwashwa mwili na huweza kusababisha kifo.
“Kasa ni moja ya kiumbe aliye hatarini kutoweka kutokana na kuliwa na binadamu ambapo kundi lao linawajumuisha Nguva,Papa Potwe,Pomboo na Nyangumi hawa wote wapo hatarini kutokweka
Aklizungumzia kuhusu sheria,Mapoy anabainisha kuwa sheria zipo na ni kali ambapo hupelekea mtu kutumikia kifungo cha miaka 10 gerezani ikiwa atakutwa na hatia.



Discussion about this post