NA MWANDISHI WETU
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, wananchi wa Kijiji cha Bucha wilayani Babati Mkoa wa Arusha wameharibu mifuko 60 ya saruji kupinga mradi wa maji katika kijiji chao.
Wananchi hao mbali na kuharibu mifuko hiyo lakini pia waliharibu jengo lililotumika kuhifadhia vifaa na kuviharibu.
Hayo yamebainishwa na Ripoti ya Mwaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG), Charles Kichere kuhusu Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2020/21.
Katika ripoti hiyo ilifafanua kuwa vurugu hizo za wananchi zilisababisha Mradi wa Maji wenye thamani ya Sh. Bilioni 7.49 kuchekelewa kutokana na vurugu zilizofanywa na wananchi wa eneo hilo kufuatia tangazo la Serikali lililotolewa Septemba 6,2019, Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dareda (Dareda WSSA) ilivunjwa na Waziri na kukabidhi majukumu yake kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Babati (BAWASA).
Ripoti hiyo iliongeza kuwa kabla ya hapo, Dareda WSSA ilikuwa ikitekeleza mradi wa usambazaji wa maji wa Dareda – Singu – Sigino na Bagara ambapo chanzo cha maji kilikuwa katika kijiji cha Bacho ambapo gharama zote za mradi zilikadiriwa kuwa Sh. bilioni 7.49 ambao ulianza Februari mosi, 2020 na ulitarajiwa kukamilika Desemba 31, 2021 huku mradi huo ulishapokea jumla ya Sh.Milioni 400 na ulikuwa umetumia Sh.Milioni 105.3.
“Kabla ya BAWASA kuanza utekelezaji wa mradi huo, ilikumbana na vikwazo kutoka kwa wananchi kutokana na wanakijiji kukataa mradi huo.
“Pia, waliharibu jengo la kuhifadhia vifaa na kuharibu vifaa vya mradi (mifuko ya saruji 60 na vyuma vilivyotakiwa kutumika kwenye mradi) vyenye thamani ya Sh. Milioni 3.052 vilivyonunuliwa kwa ajili ya ujenzi wa chanzo cha maji katika kijiji cha Bacho.
Hata hivyo ripoti hiyo ilibainisha kuwa kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa mradi ya Agosti 30, 2021, kukamilika kwa mradi kulikuwa ni asilimia 10 tu, kinyume na matakwa ya Kanuni Na. 114 ya Kanuni za Ununuzi wa Umma ya mwaka 2013 ambayo inaitaka taasisi nunuzi kuwajibika katika usimamizi madhubuti ya ununuzi wowote wa bidhaa, huduma au kazi inazozifanyia.
“Hivyo mradi ulichelewa kutokana na vurugu zilizosababishwa na jamii kutoshirikishwa ipasavyo wakati wa uanzishaji wa mradi.
“Nina mashaka na kipindi kilichosalia hadi tarehe mradi unapotarajiwa kukamilika, yaani Desemba 31,2021. Hivyo, mradi uko katika hatari ya kutokamilika kwa muda uliopangwa”ilifafanua ripoti hiyo
Kutekeleza mradi kunasababisha kuongezeka kwa gharama na hivyo inapunguza juhudi za Serikali kuhakikisha upatikanaji wa maji safi kwa jamii.
“Ninashauri menejimenti ya Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Babati (BAWASA) na Mamlaka za Mikoa ili kutatua migogoro na jamii inayowazunguka kwa kuishirikisha jamii ipasavyo ili kujenga umiliki wa mradi kwa jamii kwa maendeleo endelevu ya mradi.
“ Kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi wa Dareda-SinguSigino ili kuwezesha utoaji wa huduma ya maji kwa jamii.”ilibainisha ripoti hiyo
mwisho




Discussion about this post