NA MWANDISHI WETU
BIDHAA za tumbaku zinatajwa kuwa na kemikali zaidi ya 7,000 za sumu ambazo huingia katika mazingira kila zinapotupwa.
Tumbaku pia imetajwa kugharimu maisha ya watu zaidi ya milioni nane kila mwaka huku miti milioni 600 ikivunwa kwa ajili ya kilimo cha zao hilo.
Hata hivyo pamoja na gharama kwa binadamu,kilimo cha tumbaku huathiri hekari 200,000 za ardhi, tani bilioni 22 za maji, na tani milioni 84 za hewa ukaa au CO2 hutumiwa katika uzalishaji wa tumbaku.
Hayo ni kwa mujibu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) ambalo limeongeza kuwa sekta ya tumbaku inaathiri mazingira na afya ya watu na inahitaji kuwajibishwa zaidi kwa kusababisha uharibifu.
WHO limeeleza kwamba sekta ya tumbaku hugharimu dunia zaidi ya maisha ya watu milioni nane kila mwaka.
Gharama nyingi za kimazingira huangukia katika nchi za kipato cha chini na cha kati, ambapo maji na mashamba hutumiwa kukuza mimea ya tumbaku, badala ya uzalishaji wa chakula, ambao mara nyingi unahitajika sana.
Taarifa hiyo ya WHO yenye kichwa cha habari “Tumbaku: Kutia sumu kwenye sayari yetu” inafafanua kuwa kiwango cha hewa ukaa cha sekta hiyo kutokana na uzalishaji, usindikaji na usafirishaji wa tumbaku ni sawa na moja ya tano ya hewa ukaa inayozalishwa na sekta ya ndege za kibiashara kila mwaka, na kuchangia zaidi katika ongezeko la joto duniani.
Mkurugenzi wa Masuala ya Afya wa WHO Dk.Ruediger Krech amesema bidhaa za tumbaku ni bidhaa zilizojaa zaidi kwenye sayari, zikiwa na zaidi ya kemikali 7,000 za sumu, ambazo huingia kwenye mazingira yetu zinapotupwa.
“Takriban vichungi vya sigara trilioni 4.5 huchafua bahari zetu, mito, barabara za mijini, mbuga, udongo na fukwe kila mwaka”amesema Krech.
Aidha Krech ameongeza kuwa bidhaa kama vile sigara, tumbaku isiyo na moshi na sigara za kielektroniki pia huongeza mkusanyiko wa uchafuzi wa plastiki.
Vichungi vya sigara vina bidhaa za plastiki na huvifanya kushika nafasi ya pili ya juu ya uchafuzi wa taka za plastiki ulimwenguni.
Hata hivyo WHO imetoa wito kwa watunga sera kuvichukulia vichungi vya sigara sawa na plastiki yoyote ya matumizi ya mara moja, na kufikiria kuvipiga marufuku, ili kulinda afya ya umma na mazingira.
Mei 31 ya kila mwaka dunia huadhimisha siku ya kupinga matumizi ya tumbaku kuhamasisha jamii na watunga sera katika nchi mbalimbali duniani kuacha kilimo cha tumbaku na na matumizi ya bidhaa zake kutokana na athari za kimazingira na kiafya.
mwisho




Discussion about this post