NA GOODLUCK HONGO,
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Seleman Jaffo amewataka Mawaziri wa Maji kutoka Nchi zinazounda Bonde la Mto Nile kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi ili kulinda vyanzo vya maji.
Mbali na hilo lakini pia kuhakikisha kuwa suala la kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kulinda vyanzo vya maji liwe endelevu katika mikakati ya kila siku
Akizungumza jijini Dar es Salaam Agosti 19,2022 wakati akifungua Mkutano wa Mabaraza ya Mawaziri wa Maji wa Nchi za Bonde la Mto Nile kwa niaba ya Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, Waziri Jafo amesema ni muhimu kwa nchi hizo kulinda rasilimali za Bonde la Mto Nile ili zilete manufaa kwa wananchi wanalolizunguka.
Amesema ushirikiano ni njia bora katika kusimamia kwa amani rasilimali za maji hivyo mikutano ya Mawaziri wa Bonde la Mto Nile inatoa fursa ya kutafakari na kufanya kazi pamoja na kuweka misingi ya ushirikiano ikiwemo kutoa maelekezo ya kisera kuhusu usimamizi wa rasilimali hiyo.
Jafo ameongeza kuwa ingawa nchi zinapakana lakini maji hayana mipaka na hivyo wana kila sababu ya kulinda rasilimali hiyo ambapo hadi sasa kuna zaidi ya mabonde ya maji shirikishi 276 duniani likiwemo Bonde la Mto Nile ambapo sehemu ya mabonde hayo inachukua nusu ya ardhi ya dunia.
“Tuna kila sababu ya kulinda bonde hili na endapo chanzo hiki muhimu na adimu ambacho Mungu ametupatia endapo kitaathirika hatuna mbadala badala yake tunapaswa kukilinda na kukiendeleza na ndio maana tunafanya mikutano hii tuweze kujadiliana.
“Changamoto ya mabadiliko ya tabianchi imekuwa ni kubwa hivyo nchi zote wanachama zinapaswa kushirikiana ili kupambana nayo kwani ikiathiriki nchi moja zinaathirika zingine.

“Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inatekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ambayo inasaidia katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi”amesema Jafo
Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi wa nchi wanachama wa Bonde la Mto Nile zikiwemo Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Misri, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Sudan na Uganda.
Hata hivyo Tanzania imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo na kupokea Uenyekiti wa Baraza hilo kwa kipindi cha mwaka mmoja.




Discussion about this post