NA MIRIAM SARAKIKYA,ARUSHA.
MKUU wa Wilaya ya Monduli mkoani Arusha Frank Mwaisumbe amesema wamekamilisha zoezi la uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi kwa asilimia 100.
Mwaisumbe ametoa kauli hiyo wilayani Monduli wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu zoezi la Sensa ya Watu na Makazi inayotarajia kufanyika (kesho) Agosti 23 mwaka huu.
Amesema kwa sasa wanaendelea kuhamasisha na kutoa elimu ya Sensa ya Watu na Makazi ili Serikali iweze kuleta mandeleo kwa wananchi wake kulingana na uhitaji wao.
Aidha Mwaisumbe amebainisha kuwa wameimarisha ulinzi wa aina mbili ukiwemo ulinzi wa makarani wa sensa na vitendea kazi vyao, pamoja na ulinzi dhidi yao na wanyama wakali kutokana na Wilaya hiyo kuwa na maeneo ya hifadhi ya wanyamapori.
Mwaisumbe ameongeza kuwa sababu ya kuimarisha ulinzi huo ni kutokana na kila mwezi watu wawili au watatu hufariki kwa kushambuliwa na wanyama wakali wakiwemo tembo na chui.
Aidha amebainisha kuwa ni muhimu kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa maafisa wa sensa kwa kujibu maswali wanayoulizwa kwani zoezi la sensa ni shirikishi lakini endapo mwananchi atakataa kutoa taarifa hizo kwa hiari yake atazitoa kwa lazima kwa mujibu wa Serikali ikiwemo kutowaficha watu wenye ulemavu ndani kwani nao wana haki sawa na watu wengine.
Hata hivyo Mwaisumbe amewataka maafisa wa sensa kutumia muda na vifaa walivyopewa vizuri ikiwa ni pamoja na kuuliza maswali.




Discussion about this post