MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imesema uharibifu wa mazingira unaofanywa katika maeneo mengi nchini umesababisha wanyamapori kukosa mwelekeo na kuingia katika makazi ya watu.
Hayo yamekuja wakati ambapo kumekuwa na hali ya sintofahamu kwa wanyamapori wakiwemo Tembo kuvamia makazi ya watu katika vijiji mbalimbali nchini na kisha kuweka kambi ya muda mrefu huku wakisababisha vifo vya wananchi na uharibifu wa mali.
Akizungumzia hali hiyo,Kaimu Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kusini Mashariki kutoka TAWA,Kamishna Msaidizi Keneth Sanga amesema licha ya ulinzi mkali wa kudhibiti majangili kusaidia kuwalinda wanyamapori lakini uharibifu wa mazingira unaofanywa na binadamu unachangia hali hiyo.
“Uharibifu wa mazingira umekuwa mkubwa hali inayowafanya wanyamapori kukosa mweleko kutokana na kuharibiwa kwa mazingira”amesema Sanga
Amesema Pori la Akiba ya Selou na Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Julius Nyerere ni moja ya hifadhi kubwa barani Afrika hali inayoifanya kuwa na wanyamapori wengi ambapo kuimarika kwa ulinzi dhidi yao kunawafanya wawe huru zaidi na kufika katika makazi ya watu na kuleta madhara.
“Tembo huwa na tabia ya kutoka eneo moja kwenda lingine na hilo huwa vizazi hadi vizazi lazima wapite kwenye njia zao (Shoroba) kutoka hifadhi moja kwenda nyingine.
“Sasa humo walikokuwa wanapita miaka ya zamani sasa hivi kuna mashamba na makazi ya watu na wanapokuta mabibo,mahindi na mazao mengine huamua kuweka kambi katika eneo hilo.
“Tumefanya juhudi kubwa sana kwa sasa kuwadhibiti wanyamapori hao kwa kujenga vituo vya kudumu katika maeneo ambayo wanyama hao wamekuwa wakionekana ama kupita,lakini pia tunatoa mafunzo kwa Askari wa Vijiji maarufu kama (VGs) kuja kusaidia hali hiyo”ameongeza Sanga
Hata hivyo Sanga alifafanua kuwa mbali na kujenga vituo na mafunzo kwa VGs lakini pia wametoa namba za simu za dharula katika Vijiji vyote ili pindi wanapowaona wanyamapori katika maeneo yao basi watoe taarifa haraka.
“Tuna magari yanayofanya doria,lakini pia tuna pikipiki za askari wanaofanya doria kuhakikisha kuwa wanyamapori hao wanadhibitiwa bila madhara na kuendelea na maisha yao kwa kutoathiri maisha ya wananchi na kuharibu mazao”amesema Sanga.
Baadhi ya Mikoa ambayo Tembo wamekuwa wakifanya uharibu na kuuwa watu ni pamoja na Morogoro,Kilimanjaro Ruvuma na Lindi.




Discussion about this post