NA MWANDISHI WETU
MUUNGANO wa Asasi za Kiraia nchini wameiomba Serikali kurudisha imani na kutambua mchango wa asasi hizo katika maendeleo kwa kuwa pamoja na mambo mengine husaidia kutekeleza mipango ya maendeleo iliyotolewa na serikali.
Mbali na hilo lakini pia wameomba kufanyiwa marekebisho kwa Sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali ambazo ni pamoja na Sheria ya Utekelezaji wa haki za msingi (BRADEA), Sheria ya Makosa ya Mtandao, Sheria ya Takwimu, Sheria ya Habari, Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa, Sheria ya Uhujumu Uchumi na Utakatishaji Fedha na Sheria nyingine nyingi ambazo kimsingi zinaathiri asasi za kiraia na utendaji kazi wao
Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 30,2022 jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Asasi zingine za Policy and Legal Assistance Organization (PLAO),Tanzania Students Network Program (TSNP),Binti Makini Foundation,Her Education Foundation for Self-Reliance,Youth Solidarity for Self-Reliance (YS4S) Mkurugenzi wa Reach Out Tanzania (ROT),Kumbusho Dawson amesema lengo la taarifa hiyo ni kuhusu mazingira na tathmini ya sheria mbalimbali zinazoongoza Asasi hizo hapa nchini
Amesema Asasi za kiraia zimekuwa na mchango mkubwa kwa Taifa na zikiisaidia serikali na jamii katika kutatua changamoto mbalimbali miongoni mwao zikiwa ni changamoto ya elimu kwa umma, huduma za kijamii, ajira, msaada wa kisheria na nyingine nyingi kwa kuzingatia malengo ya kila Asasi kwa nafasi yake.
Ameongeza kuwa pamoja na mchango mkubwa wa Asasi hizo lakini zimekuwa zikikutana na changamoto za kuminywa kwa nafasi ya asasi hizo kutekeleza majukumu yao kwa uhuru, kuwepo kwa sheria nyingi kandamizi zinazolenga kuzibana na kuminya Asasi za kiraia.
Dawson amebainisha kuwa kwa kipindi cha takribani miaka sita iliyopita, Asasi za kiraia zimepitia changamoto na mazingira magumu ya kiutendaji kutokana na mitazamo ya wanasiasa na watawala,matumizi mabaya ya sheria kandamizi yaliyoambatana na mabadiliko mengi ya sheria mbalimbali zinazoongoza Asasi na washirika wake.
Aidha ameongeza kuwa baadhi ya Sheria zilizotumika na kufanyiwa marekebisho ni pamoja na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 ,Sheria za Uhujumu Uchumi na Utakatishaji Fedha,Sheria ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2002.
“Tunatoa wito kwa Serikali irudishe imani na kutambua mchango wa asasi za kiraia katika maendeleo kwa kuwa pamoja na mambo mengine husaidia kutekeleza mipango ya maendeleo iliyotolewa na Serikali.
“Viongozi, wahariri na watendaji katika vyombo vya habari wazingatie zaidi maslahi ya watanzania wanaowafikishia habari ili kuepuka kuchagua taarifa zipi ziende hewani na zipi zisiende ili mradi tu utoaji wao wa taarifa hauvunji sheria za nchi.
“Jumuiya za kimataifa hapa nchini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo na wanadiplomasia wenye ushirikiano na mahusiano mazuri na serikali kuendelea kuishauri serikali kuheshimu misingi ya utawala bora, haki za binadamu haswa uhuru wa kukusanyika,uhuru wa kupata taarifa na haki nyingine ambazo ndio msingi wa ushirikishwaji wa wananchi”amesema Dawson




Discussion about this post