NEW YORK,MAREKANI
UMOJA wa Mataifa (UN) umesema kuwa leo Novemba 15,2022,dunia itakuwa na watu bilioni nane huku India ikitarajiwa kuipita China kwa kuwa nchi yenye watu wengi zaidi duniani ifikapo mwaka 2023.
Hata hivyo zaidi ya nusu ya matarajio ya ongezeko la idadi ya watu duniani hadi mwaka 2050 litakuwa katika nchi nane ambazo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC), Misri, Ethiopia, India, Nigeria, Pakistani, Ufilipino na Tanzania.
Kwa mujibu taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini New York nchini Marekani na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema mkaazi wa bilioni nane anazaliwa kwenye sayari ambayo vita bado vinaendelea, ukosefu wa usawa unatawala, mamia ya mamilioni ya watu hawana lishe na wanakabiliwa na majanga ya mabadiliko ya tabianchi.
Guterres amesema anamatumaini kwamba katika miongo ijayo, nchi zilizo na viwango vya juu zaidi vya ongezeko la watu zitakuwa injini za maendeleo endelevu na ustawi.
“Katikati ya Novemba, idadi ya watu duniani itafikia watu bilioni nane ni ushahidi wa mafanikio ya kisayansi na uboreshaji wa lishe, afya na usafi wa mazingira,”amesema Guterres
Amesisitiza kuwa mafanikio hayo ya idadi ya watu yamegubikwa na ukweli kwamba mabilioni ya watu wanaishi katika mazingira magumu, mamia ya mamilioni wanakabiliwa na utapiamlo na hata njaa.
Amesema watu wengi wanalazimika kuacha nyumba zao, ikiwa ni pamoja na kutokana na athari za vita na majanga ya mbadiliko ya tabianchi na yote hiyo inaongeza ukuaji wa mivutano na migawanyiko.
“Iwapo hatutaziba pengo lililopo kati ya matajiri na maskini, tutajitia hatiani wenyewe kuishi katika ulimwengu wa watu bilioni nane ulioghubikwa na mivutano na kutoaminiana, migogoro na vita.”amesema Guterres
Wakati huo huo, ustawi wa idadi ya watu duniani kwa ujumla unavyoongezeka na matokeo ya afya yanaboreka lakini ukosefu wa usawa nao unaongezeka ambapo watu katika nchi tajiri zaidi wanaweza kuishi hadi miaka 30 zaidi kuliko watu katika nchi maskini zaidi.
Aidha,nchi nyingi za Kusini mwa dunia zinakabiliwa na madeni makubwa, umaskini na njaa vinaongezeka ambapo pia madhara makubwa ya ongezeko la joto duniani na hazina uwezo wa kuwekeza katika miradi endelevu ya kujikwamua.
“Hasira na kutoridhika dhidi ya nchi zilizoendelea kunaongezeka, Migawanyiko haribifu na kutoaminiana husababisha mkwamo wa masuala muhimu kuanzia upokonyaji silaha za nyuklia na ugaidi hadi afya ya umma.
“Ni lazima tuache mienendo hii yenye madhara, tujenge uhusiano na kutafuta suluhisho za pamoja za matatizo yetu ya pamoja,” amehimiza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
“kwa kuanzia, lazima tutambue kwamba ukuaji wa usawa ni matokeo ya vitendo vya ufahamu, na nchi zilizoendelea zina wajibu wa kubadili hali hii.”amesema Guterres
Awali kwa mujibu wa Ripoti ya mwaka huu wa 2022 ya Matarajio ya Idadi ya Watu Duniani iliyotolewa Novemba 11,2022 na Idara ya Umoja wa Mataifa ya uchumi na masuala ya kijamii (UNDESA) imebainisha kuwa idadi ya watu duniani inakadiriwa kufikia bilioni 8 ifikapo leo Novemba 15 mwaka huu 2022.
Ripoti hiyo ya matarajio ya Idadi ya Watu Duniani iliyotolewa katika siku yaIdadi ya Watu Duniani toleo la 27 la makadirio rasmi ya idadi ya watu ya Umoja wa Mataifa ikitoa makadirio ya idadi ya watu kuanzia mwaka 1950 hadi sasa.
Tathmini hiyo ya hivi karibuni, inazingatia matokeo ya sensa 1,758 za kitaifa zilizofanywa kati ya mwaka 1950 na 2022, pamoja na taarifa kutoka katika mifumo muhimu ya usajili na kutoka kwa sampuli 2,890 wakilishi za kitaifa kutoka maeneo au mataifa 237 duniani.
Hata hivyo taarifa hiyo imeleeza kuwa ifikapo mwaka 2023, India itaipita China kwa kuwa nchi yenye watu wengi zaidi duniani.
Aidha utafiti umeonesha Idadi ya Watu Duniani inaongezeka kwa kasi ndogo zaidi tangu mwaka 1950, ikiwa imeshuka chini ya asilimia moja mwaka 2020 lakini idadi ya watu duniani inaweza kuongezeka hadi kufikia bilioni 9.7 mwaka 2050 na kufikia karibu watu bilioni 10.4 katika miaka ya 2080 na kubaki katika kiwango hicho hadi mwaka 2100.
Vilevile taarifa imeweka wazi kuwa zaidi ya nusu ya matarajio ya ongezeko la idadi ya watu duniani hadi mwaka 2050 litakuwa katika nchi nane ambazo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC), Misri, Ethiopia, India, Nigeria, Pakistani, Ufilipino na Tanzania.
Nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zinatarajiwa kuchangia zaidi ya nusu la ongezeko la watu linalotarajiwa kufikia mwaka 2050




Discussion about this post