NA MIRIAM SARAKIKYA,ARUSHA
CHAMA cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) kimeanza kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa Kitabu cha Mwongozo wa Mashauri kwa Majaji na Mahakimu kuhusu elimu ilyokuwa katika kitabu hicho.
Rais Samia alitoa maelekezo hayo Oktoba 20,2022 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akizindua kitabu hicho na kuagiza Majaji na Mahakimu nchini kutumia kitabu cha Mwongozo wa Mashauri kwa Majaji na Mahakimu kuhusu mashauri yanayohusu ukatili wa kijinsia kama moja ya miongozo katika usikilizaji wa mashauri ya aina hiyo.
Rais Samia amesema kitabu hicho kitawapa Majaji na Mahakimu wanaosikiliza mashauri yanayohusu ukatili wa kijinsia ujasiri wa kutoa uamuzi wa mashauri hayo ambao pia utawezesha kuachwa kwa mila, desturi na imani potofu zinazokandamiza na kupora haki za makundi maalumu katika jamii ya watanzania.
“Katika kipindi cha Uongozi wangu nitahakikisha ninajenga nchi inayozingatia na kuheshimu misingi ya utawala wa sheria, haki za binadamu, na utawala bora kwa maendeleo ya nchi kiuchumi, kisiasa na kijamii”, amesema Rais Samia.
Akizungumza jijini Arusha Oktoba 13,2022 wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wakufunzi wa kitabu hicho,Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ,Joachim Tiganga amesema kuzinduliwa kwa mafunzo hayo ni ishara ya mipango iliyopangwa kwa umahiri na viongozi hao ili kuhakikisha kitabu hicho kinafundisha haki,mikataba ya kimataifa na haki za binadamu.
Jaji Tiganga amebainisha kuwa, kitabu hicho kitainufaisha jamii nzima kupitia maudhui yaliyoandikwa huku walengwa wakuu wakiwa ni wanawake na watoto.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TAWJA,Joaquine De-Mello amebainisha kuwa, wanaopatiwa mafunzo hayo wataenda kuwa walimu wa wenzao ili elimu hiyo iweze kutumika kikamilifu katika utoaji wa haki katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amesema kuwa,wanaopatiwa mafunzo hayo ni majaji na mahakimu ambao watasambaa nchi nzima kwa ajili ya kutoa elimu hiyo kuhusu kile kilichopo kwenye kitabu hicho ikiwemo masuala ya haki za wanawake na watoto pamoja na utekelezaji wa mikataba ya kimataifa na haki za binadamu.
Kwa upande wake Katibu wa TAWJA ,Anipha Mwingira amebainisha kitabu hicho kitawasaidia majaji na mahakimu kukitumia kama rejea katika kutoa maamuzi katika kesi ambazo watakuwa wanashughulikia.
Aidha amefafanua kuwa washiriki hao watapeleka elimu hiyo katika mikoa mbalimbali nchini katika kufanya rejea kuhusu masuala ya haki za ndoa,mirathi ,haki za kibinadamu na kesi zingine mbalimbali .




Discussion about this post