KINSHASA,DRC
KUNDI la pili la wanajeshi wa Kenya wamewasili katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) lililoathiriwa na machafuko na hujuma za waasi ili kudumisha amani cha baada ya Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kukubaliana kupelekwa kwa vikosi vya kikanda.
Wanajeshi hao ambao walitoka Nairobi Mji Mkuu wa Kenya na kusafiri hadi katika Mji wa Goma ni sehemu ya wanajeshi wa Kenya zaidi ya 900 ambao watakuwa nchini DRC ambapo watajiunga na wanajeshi kutoka nchi nyingine wanachama wa EAC ili kuisaidia serikali ya Kinshasa katika mapambano dhidi ya waasi ambao sasa wanadhibiti maeneo muhimu na hivyo kupelekea maelfu ya raia wa nchi hiyo kukimbia makazi yao.
Kamanda wa Kikosi cha Wanajeshi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki Meja Jenerali Jeff Nyaga ameweka wazi malengo makuu mawili ya kikosi hicho huko Kongo katika mkutano na waandishi wa habari ambapo amesema kama ninavyomnukuu:
“Tupo hapa kuulinda uwanja wa ndege wa kimataifa wa Goma dhidi ya hujuma yoyote, pamoja na makao makuu ya kikosi chetu huku michakato mingine ikiendelea.” amesema Meja Jenerali Nyaga
Kamanda Nyaga amebainisha kuwa vita haileti amani bali diplomasia inapasa kutafutwa na suala muhimu jingine linalopasa kuzingatiwa ni kuhusu kuyapokonya silaha makundi ya wanamgambo na kuyarudisha uraiani.
“Hatuwalengi waasi wa kundi la M23 pekee kwa sababu tunaona pande zote zimejielekeza kwa kundi hilo bali kuna makundi ya wanamgambo wanaobeba silaha mashariki mwa Kongo zaidi ya 120, na makundi hayo yamechochea kwa kiasi kikubwa ukosefu wa usalama katika eneo hilo. Iwapo michakato miwili hii itafeli, basi tutangia moja kwa moja katika njia ya tatu ambayo ni hatua ya kijeshi.” amesema Meja Jenerali Nyaga
Mwezi Juni,2022 Viongozi wa Jumuia ya Afrika Mashariki alikubaliana kupelekwa kwa kikosi cha kikanda huko Goma,DRC ili kukabiliana na makundi ya waasi wakiwemo M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda wakiwa wametekea maeneo makubwa huku wakiwa kilomita 20 kutoka mji wa Goma




Discussion about this post