NA MWANDISHI WETU
KATIBU Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mary Maganga amezitaka nchi za Jumuia ya Kusini mwa Afrika (SADC) kuchukua hatua za kupunguza uchomaji holela wa taka ili kuhifadhi mazingira.
Nchi hizo zinatekeleza Mradi wa Kupunguza Uzalishaji wa Kemikali Sumu aina ya uPOPs zinadumu kwenye mazingira kwa muda mrefu kutokana na uchomaji holela wa taka.
Maganga ametoa wito huo Novemba 21,2022 jijini Dar es Salaam wakati akifungua warsha kwa nchi za SADC ambazo zinazotekeleza mradi huo.
Hata hivyo,Maganga alizitaka nchi hizo kuhakikisha zinafikia malengo yaliyowekwa ya utekelezaji wa mradi huo kwa kuhuisha taarifa muhimu za kikanda zinazohusu uchomaji holela wa taka kwa kuwa na kanzidata.
Maganga amefafanua kuwa wananchi wa mataifa wanufaika wa mradi wanapaswa kuelimishwa kuhusu madhara yatokanayo na uchomaji holela wa taka na hatua zinazochukuliwa na kila nchi katika kukabiliana na athari zitokanazo na uchomaji holela wa taka.
“Malengo ya mafunzo katika warsha hii ni kukuza uelewa na ujuzi kwa washiriki kuhusu kupunguza na kudhibiti uchomaji holela wa taka pamoja na hatua za kutatua changamoto za usimamizi wa kemikali nchini na kuweka malengo ya pamoja ya kupunguza uzalishaji wa kemikali aina ya uPOPs,” amesema Maganga.
Warsha hiyo inahusisha washiriki kutoka nchi saba wananchama wa SADC zinazotekeleza mradi huo ambazo ni Botswana, Eswatini, Lesotho, Madagascar, Msumbiji, Tanzania na Zambia.




Discussion about this post