JAKARTA,INDONESIA
WAFANYAKAZI wa uokoaji nchini Indonesia wamemkuta mvulana mwenye umri wa miaka sita akiwa hai kutoka kwenye kifusi huku muda wa saa 72 muhimu za kutafuta manusura ukikaribia kumalizika baada ya tetemeko la ardhi lililotokea Jumatatu wiki hii na kuuwa watu 278..
Tetemeko hilo lenye ukubwa wa 5.6 katika kipimo cha Richter lilitokea katika jimbo la Java Magharibi ambapo Mamlaka ya majanga nchini humo imethibitisha vifo 271 hadi kufikia sasa na watu 40 wameripotiwa hawajulikani walipo huku 2,000 wakijeruhiwa.
Mamlaka hiyo iliripoti kuwa mvulana huyo ameokolewa katika wilaya ya Cianjur Novemba 23,2022.
Binamu yake aliviambia vyombo vya habari vya nchi hiyo kuwa tetemeko hilo lilitokea wakati mvulana huyo akiangalia runinga na kuongeza kuwa kulikuwa na watu watano ndani ya nyumba, yao akiwemo mvulana huyo lakini wamenusurika watatu pekee.
Katika hospitali kubwa ya Cianjur, watu wanapatiwa matibabu nje kutokana na nyufa kwenye kuta na uharibifu mwingine katika majengo hayo.
Mamlaka nchini humo zinaamini watu wengi wamekwama katika maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na tetemeko hilo.
Juhudi za uokoaji kwa kutumia mashine kubwa zimezuiwa na mitetemo na mvua ambapo karibu mitetemo 170 imetokea baada ya tetemeko la awali.




Discussion about this post