NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imekabidhi hati miliki za kimila 305 kwa wananchi wa vijiji vya Haubi na Mafai wilayani Kondoa Mkoa wa Dodoma ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula katika Maeneo kame nchini (LDSF).
Akikabidhi hati hizo Novemba 265,2022 wilayani Kondoa Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya hiyo Dkt. Hamisi Mkanacha aliishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais inayotekeleza mradi huo kwa ushirikiano na Tume ya Taifa ya Mipango na Matumizi ya Ardhi kwa kufanikisha zoezi hilo.
Amesema kupatikana kwa hati hizo ni fursha kubwa kwa wananchi wa vijiji hivyo na wilaya kwa ujumla kwani zitawasaidia kuepusha migogoro ya ardhi na kuwawezesha kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za kifedha.
Hata hivyo, Dkt. Mkanacha amewataka wanufaika wa mradi huo kuheshimu matumizi ya ardhi yaliyopangwa na kuwa ni kosa kisheria kuitumia kwa namna nyingine.
Amewaagiza viongozi wa ngazi mbalimbali wilayani humo kusimamia kikamilifu mipango ya ardhi iliyowekwa ili wananchi wasiende kinyume na kuibua migogoro.
“Ndugu zangu wananchi baadhi ya maeneo utakuta mnapanga matumzi ya ardhi lakini anatokea mtu mmoja mjuaji, mjanja anatafuta mteja anamuumizia ardhi, kwa hili tutakuwa wakali mno,” amesema Mkanacha.
Kwa upande wake Mratibu wa kitaifa wa Mradi wa LDFS Joseph Kihaule ameeleza kuwa hati miliki za kimila zinazotolewa hazihamishiki na zinabaki kwa ndugu husika hivyo hairuhusiwi kuuzwa.
Aidha ameongeza kuwa mojawapo ya faida za hati hizo ni kuwa hazitalipiwa kodi ya mwaka kama ilivyo kwa hati zingine za mijini hivyo wananchi wana fursa ya kutumia ardhi hiyo kwa maendeleo endelevu.
Akizungumzia shughuli zingine za mradi huo,Kihaule amebainisha kuwa kwa sasa vijiji vya Haubi na Mafai vinatarajia kuchimbiwa visima ili kupunguza makali ya ukame unaokabili wilaya hiyo.
Vilevile shughuli zingine kupitia mradi huo ni kuundwa kwa vikundi vya uzalishaji mali ikiwemo ufugaji wa nyuki, mifugo pamoja na uchimbaji wa visima ambavyo vikikamilika vitatumika katika umwagiliaji.




Discussion about this post