NA MWANDISHI WETU
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimempongeza hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kutunukiwa Shahada ya Udaktari wa Falsafa (Phd)ikisema hatua hiyo inadhihirisha na kusadifu kazi kubwa na anayoitekeleza kiongozi huyo mkuu wa nchi kwa watanzania.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam leo Novemba 30,2022 na Chama hicho na kutiwa saini na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka imeeleza kuwa kazi kubwa na nzuri inayofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia ni chachu ya kutolewa kwa Shahada hiyo.
“Tumeguswa na kufurahishwa na uamuzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)kumtunuku Shahada ya Udaktari wa Heshima Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan katika mahafali ya 52 duru ya 5 yaliyofanyika Novemba 30, 2022 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
“Uamuzi huo ni uthibitisho wa dhahiri wa kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Serikali ya CCM ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuleta ustawi wa maisha na maendeleo endelevu kwa nchi yetu,” imefafanua taarifa hiyo.
Aidha imeongeza kuwa kati ya kazi kubwa iliyofanyika na kutumika kumtunuku shahada hiyo ni pamoja na mageuzi ya kiuchumi, kuimarisha misingi ya demokrasia, utawala bora na kuleta maendeleo ya jamii.
“Ameleta furaha na tumaini jipya miongoni mwa wananchi. Yote hayo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 uliochagizwa na utashi wake wa kisiasa, ukomavu na umahiri alionao katika uongozi.
“Shahada hiyo ni fahari kwa Chama na Watanzania wote ikionyesha kuwa nchi ina Rais anayewajibika kwa maslahi ya wote na kwamba itampa moyo kuwa wananchi wanaona kazi nzuri anazozifanya kwa taifa hivyo kumpa ari na nguvu ya kuendelea kutekeleza wajibu wake”imebainisha taarifa hiyo
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimemtunuku Rais Samia Suluhu Hassan Shahada ya Udaktari wa Falsafa katika mahafali ya 52 duru ya tano yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amemtunuku Shahada ya Udaktari wa Falsafa wa Heshima ikiwa ni Shahada ya Udaktari wa Juu katika Humanitia na Sayansi Jamii.




Discussion about this post