ABUJA,NAIGERIA
WAZIRI wa Elimu wa Nigeria Adamu Adamu ametangaza sera yenye lengo la kukuza ufundishaji wa wanafunzi wa shule za msingi nchini humo kwa kutumia lugha za ndani badala ya lugha ya Kiingereza.
Adamu ameeleza kuwa, wanafunzi hujifunza vizuri zaidi pale wanapofunzwa kwa kutumia lugha yao mama.
Hata hivyo Waziri Adamu amekiri kuwa, kutekeleza sera hiyo mpya itakuwa na changamoto kwa sababu itahitaji kazi kubwa kuandaa nyenzo za kufundishia na kuwapata walimu ikiwemo idadi ya lugha zinazozungumzwa katika nchi hiyo zinazofikia zaidi ya 600.
Mpango huo uliopewa jina la” Sera ya Taifa ya Lugha”, tayari umepitishwa ili uanze kutekelezwa ambapo maelezo ya kufundisha wanafunzi kwa miaka sita ya kwanza katika shule za awali yatakuwa kwa lugha ya mama.
Hata hivyo, Kingereza ni lugha rasmi inayotumika nchini humo ambapo taasisi zote za kielimu hutumia lugha hiyo kama lugha ya kawaida ya kufundishia na kujifunza.
Pamoja na hayo bado haijafahamika ni lini serikali itaanza kutekeleza mfumo huo mpya wa kuachana na lugha ya Kiingereza katika shule za msingi.




Discussion about this post