MWANDISHI WETU
WAANDISHI wa Habari wameshauriwa kutumia kalamu zao katika kuibua changamoto, fursa,na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi maliasili, hasa maeneo ya shoroba ambayo ni mapito ya wanyamapori yenye muingiliano na makazi ya binadamu.
Ushauri huo umetolewa wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira(JET)Dk.Ellen Otaru wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini kuhusu uhifadhi maliasili na mazingira mapema Januari 12,2023
.“Waandishi mna nafasi na uwezo mkubwa kuelimisha jamii kuhusu uhifadhi maliasili na mazingira hasa maeneo ya shoroba ambapo ni mapito ya wanyamapori wanapoenda kutafuta maji, malisho au kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
“Shoroba nyingi zipo maeneo ya vijijini, ambapo kuna makazi ya watu, lakini kunaibuka migogoro kati ya wanyamapori na binadamu, vyanzo vya maji vinaharibiwa, watu wanalima mazao wanyamapori wanaharibu mazao.
“Hizo ni changamoto, lakini pia maeneo hayo yana fursa za kiuchumi, kijamii na kiekolojia, tumieni kalamu zenu kuyaibua hayo na kuelimisha na itasaidia jamii kuwa na mtazamo chanya,” amesema Dk. Otaru.
Kwa upande wake Meneja Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Shirika la Misaada la Marekani wa Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, John Noronha amesema maisha ya binadamu na wanyama yanategemeana, hivyo nia ni kuondoa changamoto zinazojitokeza
“Nia yetu ni kuondoa changamoto na ninyi waandishi wa habari kalamu zenu ni kama risasi mnaweza kufanya mambo makubwa, vyombo vya habari vina nguvu kuibadili jamii.
“Tufanye haya kwa faida ya uhifadhi lakini pia mazingira yetu tunayoyategemea kwa maisha yetu ya kila siku kupata hali nzuri ya hewa na shughuli za kiuchumi.”amesema Noronha
Hata hivyo Noronha amefafanua kuwa USAID kupitia mradi wake wa Tuhifadhi maliasili ulioanza Juni mwaka 2021, unafanya kazi katika shoroba saba kati ya 60 zilizopo nchini, zinazotambuliwa na Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori (TAWA).
Noronha amezitaja shoroba hizo kuwa ni Kwakuchinja, inayounganisha Tarangire na Manyara mkoani Manyara, Amani Dilu inayounganisha Misitu ya Hifadhi Amani iliyopo Muheza mkoani Tanga na Nyerere Selous Udzungwa inayounganisha Selous na Udzungwa mkoani Morogoro.
Shoroba zingine ni Ruaha Rungwa inayounganisha Itigi na wilaya ya Sikonge mkoani Tabora ikiunganisha Pori la Akiba Rungwa na Pori la Akiba Inyonga.
Nyingine ni Ruaha Rungwa Katavi, iliyopo kati ya wilaya za Tanganyika na Uvinza mkoani Kigoma, Mahale Katavi inaunganisha Hifadhi ya Taifa ya Mlima Mahale na Hifadhi ya Taifa ya Katavi na ya saba ikiwa ni Kigosi Moyowosi Burigi Chato inayounganisha mapori mawili ya Hifadhi ya Taifa Kigosi, Pori la Uwindaji Moyowosi na Hifadhi ya Taifa Burigi Chato iliyopo kati ya wilaya za Biharamulo mkoani Kagera na Kakongo Kigoma.
‘’Maeneo hayo yahikifadhiwa vizuri, nadhani Tanzania haitakosa hali nzuri ya hewa,” amesema Noronha.




Discussion about this post