NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR.
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndg.Khamis Mbeto Khamis,amekishauri Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM) kuongeza nguvu katika kudhibiti vitendo vya uhalifu baharini vikiwemo usafirishaji wa bidhaa za vyakula na rasilimali zingine kwa njia ya magendo.
Ushauri huo ameutoa Februari 2,2023 katika ziara yake ya kukagua Jahazi lenye shehena ya magendo ya mifuko ya mchele lililokamatwa na Kikosi hicho karibu na cha Kisiwa kidogo cha Tumbatu Zanzibar.
Mbeto amesema ni muhimu kwa kikosi hicho kujiimarisha zaidi kwa kufanya doria za mara kwa mara na kuimarisha kitengo chake cha kiintelijensia ili kupata taarifa sahihi za uhalifu na kuzifanyia kazi kwa haraka.
Hata hivyo Mbeto, alikipongeza Kikosi hicho kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya ya kukamata jahazi hilo lililokuwa na shehena kubwa ya mchele ambao ni zaidi ya mifuko 130 iliyokuwa ikisafirishwa kuelekea mkoani Tanga.
Amesema Zanzibar kwa sasa ipo katika changamoto ya kupanda kwa bei ya bidhaa za chakula hasa Mchele wakati kuna baadhi ya wafanyabisha wachache kwa kuendekeza tamaa wanasafirisha bidhaa hizo kwa njia ya magendo nje ya Zanzibar.
Hata hivyo Mbeto alikisihi kikosi hicho kwenda mbali zaidi kwa kushughulikia vitendo vyote vya uhalifu vinavyofanyika baharini vikiwemo usafirishaji wa dawa za kulevya,karafuu,mazao ya baharini na rasilimali zingine zinazosafirishwa kimagendo.
“Chama Cha Mapinduzi kwa sasa kipo kazini kuhakikisha kinafuatilia kwa kina utekelezaji wa Ilani yake ya mwaka 2020/2025, hivyo hakitoweza kuvumilia vitendo vya kihalifu vinavyofanywa na watu wachache”Amesema Mbeto
Naye Mkuu wa Kikosi hicho cha KMKM Zanzibar Commodore Azana Msigiri Hassan, aliahidi kupambana kikamilifu na baadhi ya watu wanaofanya uhalifu katika maeneo yote ya bahari.
Amebaisha kuwa atakuwa mstari wa mbele kulala baharini akiwasaka watu wanaofanya biashara za magendo ambazo ni kinyume cha sharia za nchi na wanaikosesha serikali mapato.
“Hivi vitendo vya magendo vinatekelezwa na watu wachache ambao ni sehemu ya wananchi hivyo natumia nafasi hii kuwaonya waache magendo na watafute shughuli halali kwani tutakayemkamata hatoweza kukwepa mkono wa sheria”Amesema Commodore Hassan.
Kwa upande wake Mkuu wa Operesheni za KMKM Kanda ya Kaskazini Unguja Ame Rashid Masema, amesema walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa Jahazi hilo lenye jina la ‘Bora imani’ lilikuwa na bidhaa za magendo mifuko 130 pamoja na watu wanne.




Discussion about this post