NA MWANDISHI WETU,TANGA
KEMIKALI na gesi zinazotumika katika majokofu, viyoyozi, vifaa vya kuzimia moto na utengenezaji magodoro ambazo huingizwa nchini kupitia mipaka mbalimbali husababisha madhara yakiwemo saratani ya ngozi, upofu na athari kwa ukuaji wa mimea na viumbe hai wengine ikiwa tazitadhibitiwa.
Mbali na hizo lakini pia ufukizaji wa udongo katika vitalu vya tumbaku, kilimo cha maua usafishaji chuma, na hifadhi ya nafaka katika maghala navyo vimetajwa kusababisha madhara hayo.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Catherine Bamwenzaki ametoa taarifa hiyo Februari 10, 2023 wakati akifungua mafunzo kwa maafisa wa Serikali waliopo katika mpaka wa Horohoro mkoani Tanga, kuhusu udhibiti wa uingizaji nchini wa gesi na vifaa vyenye gesi zinazomong’onyoa tabaka la ozoni.
Amesema ni muhimu kwa wasimamizi wa sheria waliopo katika mipaka kusimamia na kudhibiti gesi zinazochangia kumong’onyoa tabaka la ozoni pamoja na kuchangia ongezeko la kiwango cha joto duniani na kusababisha mabadiliko ya tabianchi.
“Kemikali na gesi zinazotumika katika majokofu, viyoyozi, vifaa vya kuzimia moto,utengenezaji magodoro,ufukizaji wa udongo katika vitalu vya tumbaku, kilimo cha maua,usafishaji chuma, na hifadhi ya nafaka katika maghala husababisha madhara yakiwemo saratani ya ngozi, upofu na athari kwa ukuaji wa mimea na viumbe hai wengine”amesema Bamwenzaki
Ameongeza kuwa ni lazima kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuhifadhi tabaka la ozoni ambalo kama likimong’onyoka huruhusu mionzi zaidi ya urujuani kufikia uso wa dunia ambayo huathiri afya ya binadamu na mazingira
Aidha amebainisha maafisa hao wa mipakani watumike kuhamasisha matumizi ya gesi mbadala ambazo ni rafiki kwa afya ya binadamu na mazingira.
Bamwenzaki ameongeza kuwa mwanzoni mwa miaka ya 1970 wanasayansi walivumbua kwamba baadhi ya kemikali zinazotengenezwa na binadamu hujipenyeza angani na kumong’onyoa tabaka la ozoni na uchunguzi wa angahewa tangu miaka hiyo umethibitisha kwamba tabaka la ozoni limekuwa likimong’onyoka kwa kasi ya asilimia tano kila muongo.
Aidha ameeleza kuwa matokeo ya uvumbuzi huo yamesababisha Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) kufanya tathmini ya kisayansi mwaka 1976 na kuchukua hatua kulinda tabaka hilo.
“Chini ya Programu ya Taifa, Serikali pia imeandaa na inatekeleza Mpango wa Kuondosha Kemikali Zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni Jamii ya Hydrochlorofluorocarbons (HCFCs) ifikapo mwaka 2030.
“Na chini ya mpango huu mojawapo ya shughuli zinazotelekezwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa maafisa Forodha na Wasimamizi wa Sheria nchini kuhusu utekelezaji wa Kanuni za Usimamizi wa Mazingira yaani Udhibiti wa Kemikali Zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni za mwaka 2022 na utekelezaji wa Mikataba ya Vienna na Montreal Nchini.”amesema Bamwenzaki
Kwa upande wake Afisa Mfawidhi wa Forodha Kituo cha Horohoro Odero Ryoba ameishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kutoa mafunzo hayo akisema yataleta tija katika majukumu yao.
Odero ameiomba Serikali kuendelea kutoa mafunzo kwa maafisa katika vituo vyote nchini ya kutambua kemikali haribifu kwa tabaka la ozoni ili iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Katika mafunzo hayo washiriki wameelimishwa kuhusu Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (Kanuni za Kudhibiti Kemikali Zinazoharibu Tabaka la Ozoni), 2022.
Mada nyingine ni athari zitokanazo na uharibifu wa tabaka la ozoni & Udhibiti wa uingizaji nchini wa kemikali zinazodhibitiwa chini ya Itifaki ya Montreal na Matumizi ya Mitambo ya Kutambua Gesi zinazoharibu Tabaka la Ozoni ambapo jumla ya maafisa wa serikali 720 kutoka mamlaka mbalimbali za udhibiti wamepatiwa mafunzo.




Discussion about this post