NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM)kimewataka wanasiasa na wanachama wa vyama vya upinzani nchini kuacha kauli za uchochezi wa vurugu na badala yake wajielekeze katika kudumisha amani na mshikamano.
Mbali na hilo lakini pia kimesema hakuna mtu yeyote mwenye hati miliki ya Chama hicho bali ni chama cha watu wote.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Mohammed Said Mohammed (Dimwa),wakati akizungumza na maelfu ya wanachama wa chama hicho katika ofisi ya chama hicho Kitengo cha Uratibu Chachani Chake Chake kisiwani Pemba.
Amesema, kumeanza kujitokeza maneno na CCM msimamo wake ni kujibu maneno hayo kupitia usimamizi wa utekelezaji wa Ilani yake ya mwaka 2020/2025 inayotekelezwa kwa kasi kubwa na Serikali zote mbili ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kazi yetu kubwa ni kuwahudumia wananchi waliotupa kura za kuongoza dola, hatuwezi kukatishwa tamaa na kauli za baadhi ya wasioitakia mema CCM.
“Tunawaonya baadhi ya wanasiasa na wanachama wa vyama vya upinzania nchini kuacha kauli za uchochezi wa vurugu na badala yake wajielekeze katika kudumisha amani na mshikamano.
“Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) inatambuliwa ndani ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984,hivyo wasioridhika wana nafasi ya kufuata taratibu ili kama kuna changamoto zitatuliwe.”,amesema Dkt. Dimwa.
Aidha amewatataka viongozi na wanachama wa CCM kuwa na mipango kazi inayoendana na mikakati ya kuimarisha chama hicho.
“Naamini kuwa Chama cha Mapinduzi 2025 kitashinda kwa kishindo tena saa nne asubuhi kwani tuliyoahidi tunaendelea kuyatekeleza kwa vitendo”.amefafanua Dkt.Dimwa.
Aidha amefafanua kuwa CCM itafanya siasa za kisayansi kwa kuhakikisha kila mwanachama ananufaika na fursa zinakazopatikana kupitia taasisi hiyo kubwa ya kisiasa.
Hata hivyo amewatoa hofu baadhi ya wananchi wanaokosoa maamuzi ya Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuruhusu mikutano ya hadhara kwani Viongozi wa Chama na Jumuiya zake wana uwezo wa kujibu hoja hizo kwa ufasaha.
“Nina kazi mbili kubwa kwanza ni kumtetea Mwenyeti wa CCM, kumsemea lakini na kumlinda, na ya pili ni kumlinda na kumsemea Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Rais Dk.Hussein Mwinyi.”amebainisha Dkt.Dimwa
Dk.Dimwa ameongeza kuwa wakati umefika wa Chama hicho kurudi kwa wanachama wenyewe ili waamue masuala mbalimbali yenye tija ya kisiasa na kiuchumi. hakuna mtu yeyote mwenye hati miliki ya Chama hicho bali ni chama cha watu wote.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kusini Pemba, Yussuf Ali Juma ameahidi kutoa ushirikiano na kutekeleza maelezo yote yaliyotolewa.
Kwa upande wake Katibu wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba Inocent Nyanzaba, amesema hali ya kisiasa ndani ya Mkoa huo ipo vizuri.
Awali Mkuu wa Mkoa huo Mantar Zahor Masoud, amesema wametekeleza kwa ufanisi Ilani ya CCM kwa kuimarisha huduma za afya,maji,elimu,uvuvi,kilimo,biashara na mindombinu ya usarifi wa anga na nchi kavu
“Katika juhudi za kuwawezesha wananchi kiuchumi serikali imetoa jumla ya Sh.Bilioni nne kwa ajili ya mikopo ya kuviwezesha vikundi 45.
“Pamoja na mafanikio haya,tunakabiliwa na changamoto ya upungufu wa huduma za maji safi na salama kwa baadhi ya maeneo,ambayo inasababishwa na umeme kuwa na nguvu ndogo za kuendesha mitambo ya maji”amefafanua Masoud
Akijibu hoja hiyo, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis, amefafanua kuwa CCM tayari imeanza kuchukua juhuzi za kuzungumza na viongozi wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) ili wakutane na viongozi wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kwa ajili ya kumaliza changamoto hiyo kisiwani Pemba.




Discussion about this post